Aika Swai, New York, USA
"Sisi tunaoishi nje tunawaomba kina baba na mama, kaka na dada mumpe kura zenu
Kikwete na Karume. Maisha bora kwa kila mtanzania."
» Home
» Habari Mpya » Ngawaiya awaponda wanaobeza baraza jipya la mawaziri
Ngawaiya awaponda wanaobeza baraza jipya la mawaziri
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kilimanjaro, Thomas Ngawaiya, amewajia juu wote wanaolibeza Baraza la Mawaziri la serikali ya awamu ya nne lililoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete.
Ngawaiya ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari wa mjini Moshi, alisema wengi wa watu hao wana wivu binafsi na kwamba siyo watu wenye kutaka Tanzania ijikwamue na umaskini.
Alisema wakati baadhi ya watu hao wanalalamikia kuundwa kwa wizara mpya kadhaa kama vile za Miundombinu, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Usalama wa Raia, yeye anaona uamuzi wa rais kuunda wizara hizo unastahili kuungwa mkono badala ya kulalamikiwa. "Wengi wanaolinyanyapaa Baraza la Mawaziri la awamu ya nne kuwa lina mawaziri wengi au kwa nini wanawake wamepewa nafasi nyeti au litatumia fedha nyingi za serikali mimi nadhani hawaoni mbali, wanadhani Tanzania ya mwaka 1995 ndiyo hii ya mwaka 2006," alisema.
"Nadhani bado watu hao japokuwa wana haki yao kikatiba ya kutoa mawazo lakini hawajaeleza sababu za msingi za kupinga Baraza hilo...naamini wanalionea wivu kwa jinsi lilivyo baraza zuri na makini," aliongeza Ngawaiya.
Aliwataka wanaodai kuwa Baraza la Mawaziri la Kikwete ni kubwa mno kwa idadi ya mawaziri na wizara wakajifunze nchi nyingine kama vile Bangladesh, ambayo ina waziri anayeshughulikia zao moja tu la 'jute' (katani).
"Wanaopinga Baraza la Kikwete waende Bangladesh wakajionee...mimi nimefika huko nimekuta kuna Waziri anashughulikia zao moja tu la Katani, hakuwa Waziri wa Kilimo, ni waziri wa zao la katani tu...sasa hapa Tanzania, Rais Kikwete kaunda wizara ya kukabiliana na majambazi au ya Afrika Mashariki tu, kakosea nini? alihoji Ngawaiya.
Alisema kuundwa kwa wizara inayohusiana na masuala ya polisi ni faraja kwa wananchi ambao kwa sasa watahudumiwa kwa ufanisi mkubwa na jeshi hilo.
Ngawaiya maarufu mjini hapa kwa jina la Kada wa CCM alisema wizara mpya ya Afrika Mashariki itawezesha Watanzania kufaidi matunda ya Ushirikiano wa nchi tatu za Tanzania,Kenya na Uganda.
"Wapo wasomi wanathubutu kusema kuwa Wizara ya Afrika Mashariki ingepaswa kuwa kitengo ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje, hizo ni fikra ndogo na hazifai kuungwa mkono na watu wenye upeo mkubwa wa mawazo," alisema kwa kujiamini.
Amewapongeza wote walioteuliwa kuwa Mawaziri au Naibu Waziri na vile vile amemwagia sifa Rais Kikwete na washauri wake waliomsaidia kuunda baraza hilo la mawaziri na kwamba amewaomba Watanzania waache malumbano ya kisiasa na kuipa ushirikiano wa hali na mali serikali.
Alisema ushirikiano wa wananchi ndio utakaomsaidia Rais Kikwete kutimiza ahadi zake alizowapa wananchi wakati wa kampeni zake za kuwania Urais mwaka jana.