Asema taifa linaweza kukumbwa na matatizo
RAIS Jakaya Kikwete amesisitiza kwamba Tanzania lazima iendelee kujiepusha kuchanganya dini na siasa kwa gharama yoyote.
Alikuwa akitoa mhadhara juzi jioni katika Chuo Kikuu cha Boston, Marekani, uliohusu ‘Menejimenti ya Tofauti za Kidini katika Mazingira ya Kidemokrasia; Uzoefu wa Tanzania’. Miongoni mwa watu mashuhuri waliosoma hapo ni marehemu Dk. Martin Kuther King.
Rais Kikwete alitahadharisha kuwa kuchanganya dini na siasa kunaweza kulitumbukiza taifa katika matatizo makubwa bila sababu za msingi.
Alisema dunia hivi sasa, kitaifa na kimataifa, inakabiliwa na changamoto kubwa ya namna ya kukabiliana na tofauti za kidini kuliko wakati mwingine wowote.
Rais alisema hakuna chaguo lingine la kufanya zaidi ya kufanya kazi kwa bidii, kuhimiza na kuendesha mijadala ya kati ya dini na dini na kuhimiza kuvumiliana na kuelewana, wakati yakishughulikiwa matatizo yanayotokana na vitendo vyenye dalili za kigaidi na mifarakano ya kisiasa.
Akikatishwa mara kwa mara kwa kofi kutoka kwa wanafunzi, menejimenti ya chuo na wageni mbalimbali, akiwemo Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, ambaye anasoma katika Chuo Kikuu cha Harvad, alisema kwa uzoefu wa Tanzania jambo hilo linawezekana.
Alisema masuala yanayohusu imani mara zote yamekuwa na mwelekeo wa kuwagawa watu katika misingi ya ‘wao na sisi’ na mbaya zaidi katika misingi ya ‘wale wanaoamini na wasioamini’, na kuonya kuwa kama migawanyo hiyo haitaeleweka na kuchukuliwa vizuri, inaweza kuwa na matoko mabaya.
Alifafanua kuwepo uhuru wa kuhubiri dini, lakini bila ya kutumia mwanya huo kukashifu dini ya mwingine, na hivyo kujenga mizizi ya umoja wa kitaifa na maelewano.
Rais alisema katika kujenga misingi ya utawala bora Tanzania, hata uanzishwaji wa vyama vya siasa umewekewa taratibu za kisheria na kutojielekeza kuanzishwa kwa misingi ya kidini.
Katika mhadhara huo, ambao uliandaliwa na Taasisi ya Utafiti inayoshughulika na viongozi wastaafu wa Afrika, ikiongozwa na aliyewahi kuwa balozi wa Marekani nchini Tanzania, Charles Stith, Rais Kikwete alibainisha kuwa Tanzania imeweza kuwa na menejimenti nzuri ya tofauti za kidini katika mazingira ya kidemokrasia kutokana na misingi mizuri aliyoweka Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Nyerere.