HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA EDWARD LOWASSA (Mb), WAKATI WA KUTOA HOJA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA TANO WA BUNGE, DODOMA TAREHE 15 NOVEMBA, 2006
Mheshimiwa Spika, Tumefika mwisho wa kazi za mkutano wa tano wa Bunge lako Tukufu. Mkutano huu wa tano ndio vilevile unaohitimisha mwaka wa kwanza wa uhai wa Bunge hili na Serikali ya awamu ya nne. Mwaka sio kipindi kirefu, lakini vilevile unaashiria kuwa muda unakwenda na kwamba hautusubiri. Tunao wajibu kuendelea kujikumbusha kuwa majukumu tuliyo nayo mbele yetu bado ni mengi na yanahitaji kutekelezwa kwa ari na nguvu. Katika mkutano huu jumla ya maswali 165 ya msingi pamoja na mengine mengi ya nyongeza yaliyoulizwa na Waheshimiwa Wabunge yalijibiwa na Serikali. Aidha, katika mkutano huu, Wabunge waliweza kujadili na kuridhia maazimio saba. Miongoni mwa maazimio hayo ni lile la kuridhiwa kwa Mkataba wa Kuondoa Matumizi ya Viza kati ya Tanzania na Msumbiji. Kwa kuridhia Azimio hilo, Bunge lako Tukufu limeonyesha dhahiri umuhimu wa kuendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji. Aidha, ni kielelezo kwamba wananchi wa nchi hizi mbili ni ndugu na kwamba mpaka uliopo ni wa kiutawala tu na hauwazuii kuendeleza na kudumisha uhusiano wao.
Mheshimiwa Spika, na mimi napenda kuungana na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza Mheshimiwa Ali Ameir Mohamed, Mbunge wa Donge, kwa kuchaguliwa kuwa Katibu wa Kamati ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi. Aidha, katika mkutano huu Waheshimiwa Wabunge waliwachagua Wabunge wa kuiwakilisha nchi yetu katika Bunge la Afrika Mashariki. Napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Bunge la Afrika ya Mashariki. Mheshimiwa Dkt. Didas John Massaburi, Mheshimiwa Dkt. George Francis Nangale, Mheshimiwa Dkt. Aman Walid Kabourou, Mheshimiwa Dkt. Fortunatus L. Masha, Mheshimiwa Abdullah Ali Hassan Mwinyi, Mheshimiwa Dkt. Saidi Gharib Bilal, Mheshimiwa Kate Sylivia Kamba, Mheshimiwa Janeth Deo Mmari na Mheshimiwa Sebtuu Mohamed Nassoro. Wote hawa ni wasomi wazuri. Tunawategemea waweze kusukuma ajenda zitakazotuwezesha kujenga Jumuiya ya Afrika ya Mashariki yenye maslahi kwa nchi zote na hasa yale ya Tanzania. Watatusaidia kuwahakikishia Watanzania kuwa tusiogope kujiunga na wenzetu, bali tujizatiti kutumia fursa zilizopo na zitakazojitokeza ndani ya jumuiya kunufaika kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Spika, tarehe 13, Oktoba 2006 Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, alizindua kamati ya Kitaifa ya Kukusanya maoni ya Watanzania kuhusu mchakato wa kuangalia uwezekano wa kuharakisha Shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki. Naomba wananchi wote wajitokeze kwa wingi kutoa maoni mbele ya kamati kadri itakavyokuwa inazunguka maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Aidha, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na viongozi wengine watoe ushirikiano kwa Kamati hiyo na wawahamasishe wananchi ili waweze kujitokeza kwa wingi kutoa maoni ambayo yataisaidia sana Serikali katika kufanya uamuzi.
Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu liliweza kujadili na kupitisha jumla ya miswada sita (6). Miswada hiyo ni Muswada wa Sheria ya Kufanya Marekebisho kwenye Sheria mbalimbali ya mwaka 2006. Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Kanuni ya Adhabu, sura ya 16; Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20; Sheria ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, sura ya 391; Sheria ya Vyama vya Siasa, sura ya 258; Sheria ya Uchaguzi, sura ya 343 na; Sheria ya Taasisi ya Kazi ya 2004, Na. 7 ya mwaka 2004; na Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004. Aidha, Waheshimiwa Wabunge waliweza kujadili na kupitisha Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2006. Sheria hiyo mpya inakusudia kuubadili mpango uliopo wa akiba unaoendeshwa kwa ajili ya wafanyakazi wa Serikali za Mitaa, taasisi zinazohusiana nazo na wachangiaji wengine na kuufanya kuwa mfumo wa pensheni kwa ajili ya walengwa hao na wengine watakaopenda kuchangia kwa mujibu wa maelekezo ya Sheria. Lengo ni kutoa mafao mazuri zaidi kwa wanachama walio katika mfumo wa pensheni.
Bunge pia lilipitisha Muswada kuhusu marekebisho katika Sheria mbalimbali za Serikali za Mitaa. Marekebisho hayo yanakusudia kuwezesha Halmashauri kuendelea kuwa na mamlaka katika eneo lililobaki baada ya kuundwa Halmashauri mpya. Marekebisho pia yanakusudia kuwafanya wabunge wa kuteuliwa na Rais na wajumbe wanaoteuliwa na Waziri kuwa wajumbe wa Halmashauri za Wilaya wanazoishi. Marekebisho haya yanaweka muda ambao wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya watakaa madarakani, kuanzisha Ofisi na majukumu ya Katibu Tarafa na mapendekezo mengi mengine ambayo yote Waheshimiwa Wabunge mmeyakubali.
Muswada Kuhusu Utoaji Huduma za Mawasiliano uliopitishwa na Bunge lako Tukufu una lengo la kuweka utaratibu, mwongozo, usimamizi na utoaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijiji. Madhumuni ya Muswada ni kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Huduma za Mawasiliano ili kuweza kuwafikia wananchi wengi hususan wale wanaoishi vijijini na kwenye maeneo ambayo hayana maslahi kwa msingi wa biashara. Aidha, Bunge lako Tukufu lilipitisha Muswada wa Sheria ya Nyama wa mwaka 2006 (The Meat Industry Bill, 2006) na Muswada wa Sheria ya Udhibiti wa Biashara ya Fedha Haramu wa mwaka 2006 (The Anti-Money Laundering Bill, 2006). Biashara ya fedha haramu ni tatizo kubwa la dunia ya leo. Nchi nyingi duniani zimeamua kushirikiana katika kupambana na mbinu za kisasa, matumizi ya wataalamu na wanataaluma mbalimbli katika kuficha umiliki na mapato haramu. Kwa kuzingatia hayo, kupitishwa kwa muswada huu kuwa Sheria kutatuwezesha kuwa na muundo madhubuti na hatua za kupambana na tatizo la biashara ya fedha haramu nchini. Napenda kulipongeza Bunge lako Tukufu na wadau mbalimbali waliofanikisha kazi ya kujadili na kupitisha miswada yote hiyo.
Mheshimiwa Spika, wakati wote Bunge lako Tukufu linapopitisha miswada tunaweka misingi na taratibu za kutuwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisiasa tunazokumbana nazo tunapotekeleza mipango yetu ya kuwawezesha wananchi kuwa na maisha bora zaidi. Kama ambavyo Bunge hili limedhihirisha hadi hivi sasa, upo mshikamano na maelewano kati ya Bunge, Serikali na wadau wengine wengi waliotoa michango yao ya mawazo katika kuwezesha kupitishwa kwa miswada hiyo.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha takriban mwaka mmoja tangu aingie madarakani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ametumia uwezo wake na fursa mbalimbali zilizojitokeza, kuweka mazingira ya kuwezesha washiriki wengi zaidi wa maendeleo yetu kujitokeza na kushirikiana nasi katika kufikia malengo tuliyojiwekea. Ziara zake zimekuwa na malengo maalum na kila nchi aliyotembelea amejenga hoja ya ushirikiano katika utatuzi wa kero mbalimbali zinazokwamisha maendeleo yetu. Katika ulimwengu wa sasa, fursa za maendeleo kimataifa zipo, lakini zinahitaji viongozi wanaothubutu na wanaozifuata. Rais wetu ameonyesha dhamira hiyo. Tumuunge mkono kwa dhati. Rais wa Benki ya Dunia, Paul Wolfowitz hivi karibuni alieleza kuwa katika kipindi cha miezi 16 alichokaa madarakani ndani ya Benki ya Dunia ameona jitihada za kuridhisha za baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika ambao wana dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo katika nchi zao. Kwa maneno yake anasema (nanukuu):
�We are seeing an informed African Citizenry increasingly demanding change. We are seeing leadership that is increasingly aware of it�s responsibility to its people. Leadership that pushes for reforms and in some cases does so at significant personal risk�.
Rais huyo wa Benki ya Dunia anazitaja Tanzania na Ghana kuwa miongoni mwa nchi kumi duniani zinazotambuliwa kimataifa kuwa zipo katika mstari wa mbele kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wake. Kwa hiyo, tusilegeze kamba. Pamoja na matatizo tunayokumbana nayo na hasa hili la umeme tuuanze mwaka wa pili wa Serikali ya awamu ya nne kwa kasi ile ile.
Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Novemba, 2006 Benki ya Dunia ilizindua taarifa yake ya mwaka inayoelezea vigezo mbalimbali vya maendeleo ya Afrika (Africa Development Indicators 2006) na kubainisha changamoto zinazokabili Bara la Afrika. Taarifa hiyo ya Benki ya Dunia na utafiti uliofanywa umeibua changamoto nne kubwa za kukuza uchumi wa Bara la Afrika ambao watafiti wanaziita kwa kifupi �The four big �I��s needed to achieve growth in Africa. That is Infrastructure, Investment, Innovation and Institutional Capacity�. Kwa maneno mengine ni kuwa maeneo muhimu yaliyobainishwa ambayo yanahitaji msukumo wa kipekee wa Serikali na wadau wake wote wa maendeleo ni kuhusu:
- Kuongeza kasi ya uwekezaji katika miundombinu,
- Kuboresha mazingira ya uwekezaji rasilimali;
- Kuimarisha na kukuza ubunifu;
- Kujenga uwezo wa kitaasisi; na
- Utawala bora
Mheshimiwa Spika, maeneo haya manne ni muhimu sana katika kutuwezesha sisi Watanzania kukuza uchumi na kupiga vita umaskini. Dhamira ya Serikali ni kufikia malengo hayo kwa kasi na kwa haraka. Katika taarifa hiyo hiyo ya Benki ya Dunia, zipo takwimu zinazoonyesha viashiria mbalimbali vya maendeleo Barani Afrika. Ingawa takwimu zilizotumika kwenye taarifa hiyo ni za mwaka kati ya 1996 � 2005 napenda kuelezea baadhi ya vigezo ili vituwezeshe kujipima na hivyo kutupa changamoto ya kuongeza kasi ya maendeleo yetu:
(a) Wastani wa Ukuaji wa Pato la Taifa
(1996 � 2005)
Msumbiji asilimia 8.4
Angola asilimia 7.9
Sudan asilimia 6.4
Uganda asilimia 6.1
Botswana asilimia 5.7
Ethiopia asilimia 5.5
Tanzania asilimia 5.4
Ghana asilimia 4.7
Malawi asilimia 3.2
Kenya asilimia 2.8
Zimbabwe asilimia 2.4
(b) Wastani wa Umri wa Kuishi
(life expectancy)
Seychelles miaka 73
Mauritius miaka 72
Ghana miaka 57
Kenya miaka 51
Uganda miaka 50
Tanzania miaka 48
Msumbiji miaka 45
Zambia miaka 40
Swaziland miaka 37
(c) Kiwango cha Uandikishaji watoto shule za msingi (Net Enrolment ratio)
Seychelles asilimia 100
Uganda asilimia 98
Malawi asilimia 95
Afrika Kusini asilimia 89
Tanzania asilimia 86
Kenya asilimia 76
Msumbiji asilimia 71
Ethiopia asilimia 46
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio tuliyoyapata mwaka jana ya kuwa na viwango vizuri vya ukuaji katika baadhi ya vigezo vya uchumi kama vile Pato la Taifa, bado tuko nyuma. Kwa kuzingatia ulinganisho huo kati yetu na baadhi ya nchi nilizozitaja ni dhahiri kuwa tunahitaji kuongeza kasi zaidi. Dhamira ya kasi mpya ni kuondoka tulipo sasa kwenye viwango vidogo vya kimaendeleo. Tuwanie kushika nafasi za juu zinazotuwezesha kuondoa umaskini kwa haraka. Hatua zinazochukuliwa na Serikali sasa zina lengo hilo. Kwa mfano, kutoa msukumo katika elimu, afya, barabara na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Hivyo, hatuna budi kama Taifa tubadilike. Dhamira ya kasi mpya ndiyo itatufikisha huko tunakotaka. Viongozi na wananchi lazima tubadilike kifikra, na tuwe na nidhamu katika shughuli zetu za kila siku.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kutumia nguvu na rasilimali zetu ni vema tuzingatie mazingira ya kimataifa katika mchakato wa maendeleo yetu. Zipo fursa nyingi za Tanzania kujiletea maendeleo kwa haraka katika Jumuiya ya Kimataifa ambazo hata hivyo, bado wananchi wetu wengi hawajaelimishwa vya kutosha namna ya kuzichangamkia na kuzitumia ili kuondokana na umaskini. Hivyo, natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge kuwaelimisha wananchi kuhusu fursa nyingi za ndani na nje na namna ya kuibua miradi itakayowawezesha kufaidika.
Mheshimiwa Spika, napenda nitumie mfano wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kusisitiza hoja yangu. Sote tunajua kuwa Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kuboresha huduma za jamii ikiwa ni hatua mojawapo ya kupambana na umaskini kwa kusaidia shughuli za wananchi katika sekta za afya, elimu, maji, miundombinu, mazingira na mafunzo.
Awamu ya kwanza ya Mfuko huo iliyoanza mwaka 2000 ilikuwa na mafanikio mengi. Miongoni mwa mafanikio hayo ni kutekelezwa kwa miradi 1,399 ya Jamii na miradi 305 ya ujenzi hususan ujenzi wa vyumba vya madarasa 2,586, Ofisi za walimu 468, nyumba za walimu 335, maabara 18, majengo ya zahanati na vituo vya afya 312, nyumba za waganga wasaidizi na wauguzi 922, kugharamia matengenezo ya barabara kadhaa vijijini, kuchimba visima vya maji na kugharamia mafunzo ya watendaji wa Halmashauri. Kutokana na mafanikio hayo Wahisani waliafiki mpango huo wa TASAF uingie awamu ya pili mwaka 2005/2006. Katika awamu ya pili mpango huo unazishirikisha Halmashauri zote nchini pamoja na Unguja na Pemba. Lengo la miradi hii ni kusukuma kwa kasi zaidi vita dhidi ya umasikini katika ngazi ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni katika vyombo vya habari, Kamati ya Usimamizi ya TASAF Taifa inayosimamia awamu ya pili ya mradi huu, ilitoa taarifa kuwa imeidhinisha utekelezaji wa miradi 453 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 10.7. Fedha za miradi hiyo zimetumwa kwenye Halmashauri ambazo zimewasilisha TASAF makao makuu maombi ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi iliyobuniwa na jamii.
Serikali inaamini kuwa fedha hizi zitasaidia jitihada za kukuza uchumi na kuondoa umaskini kule walipo wananchi. Hata hivyo, inasikitisha kuona kuwa hadi tarehe 8 Novemba, 2006, Halmashauri 22 zilikuwa bado hazijawasilisha maombi ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya TASAF. Halmashauri hizo ni Kishapu, Kibaha, Temeke, Kondoa, Bukoba Manispaa, Bukoba Vijijini, Karagwe, Ngara, Biharamulo, Moshi, Liwale, Ngorongoro, Tarime, Babati Mji, Babati Vijijini, Hanang, Morogoro Manispaa, Mtwara, Iramba, Lushoto na Korogwe.
Mheshimiwa Spika, uzoefu wa mchakato mzima wa kuibua na kuidhinisha miradi ya TASAF na pia katika ziara za viongozi wa Serikali mikoani, imebainika kuwa upo udhaifu wa baadhi ya watendaji wa Halmashauri katika miradi hii. Wataalam na hata baadhi ya viongozi hawapo makini kusaidia wananchi kuibua miradi ya maendeleo inayokidhi viwango na vigezo vya kupata fedha. Hali hii hairidhishi kwani fedha zipo, miradi ya wananchi ipo, lakini miradi haiibuliwi katika ngazi ya Halmashauri. Mfano: Zipo taarifa kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Temeke hadi sasa haijaipeleka Makao Makuu ya TASAF miradi ipatayo 23 iliyoibuliwa na wananchi kwa sababu wanasubiri Kata moja iliyochelewa nayo iibue mradi wake na kuuwasilisha. Tunajiuliza tatizo ni nini?. Maamuzi ya aina hiyo yanachelewesha maendeleo ya wananchi wetu.
Napenda nitoe mfano mwingine, Katika ziara niliyofanya mkoani Iringa Mwezi Septemba, 2006 tatizo la kasi ndogo ya kuibua miradi ya wananchi vijijini lilijitokeza pia. Taarifa ya mkoa ilieleza kuwa chini ya Programu ya Kilimo inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA) ambayo inajulikana kama Agricultural Sector Program Support (ASPS-II) kuanzia Januari mwaka 2005 hadi Juni 2006 jumla ya shilingi milioni 503 zilizokuwa zimetengwa kwa miradi ya Halmashauri mbalimbali za mkoa wa Iringa hazikutumika kwa sababu miradi haikuibuliwa. Vilevile Mwaka huu, mradi ulitengewa shilingi 4.7
bilioni na kati ya fedha hizo, tulielezwa kuwa hadi mwezi Septemba, 2006 kiasi kilichotumika ni asilimia 33.7 tu. Kutokana na udhaifu huo wa kuibua miradi, ilibidi shilingi 736.6 milioni ziachwe mkoani (unallocated) ili zitumike kushindanisha Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kasi ndogo ya kuibua miradi ya wananchi vijijini napenda kusisitiza mambo yafuatayo:-
(i) Viongozi wa mikoa kwa kushirikiana na Halmashauri ziwe na mkakati wa pamoja wa kusaidia wananchi vijijini kuibua miradi mizuri ya maendeleo hususan kupitia programu ya TASAF, ASDP na programu nyingine za Serikali.
(ii) Viongozi katika ngazi ya Halmashauri waache mivutano ya kisiasa ya kuchelewesha miradi kutokana na ubinafsi wa kila mtu kutaka mradi wa kata yake uwe wa kwanza kupata fedha hata kama haukidhi vigezo.