Mheshimiwa Spika: Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uhai na afya, na akatukutanisha hapa, Ninamshukuru pia kwa Uchaguzi Mkuu wa amani, utulivu na heshima kubwa kwa nchi yetu.
Nakishukuru sana Chama changu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa heshima kubwa kilichonipa kwa kuniteua niwe mgombea wake wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ninawashukuru wananchi kwa kunipa mimi na chama changu ushindi mkubwa sana. Shukrani zangu kwa Watanzania wenzangu--wana-CCM na wasio wana-CCM ni ahadi ya kuwatumikia kwa uwezo wangu wote.
Nawashukuru wapinzani kwa ujasiri wao mkubwa wa kujitokeza kushindana na chama cha Mapinduzi. Uchaguzi sasa umekwisha. Kauli ya wananchi imedhihirika. Tuungane, tuwe kitu kimoja; tujenge na kuendeleza nchi yetu.
Nawashukuru waheshimiwa Wabunge kwa kumkubali mteuliwa wa CCM kwa nafasi ya Spika, Mheshimiwa Samuel John Sitta, Mb., na pia kwa kukubali uteuzi wangu wa Waziri Mkuu, pamoja na Mawaziri na Naibu Mawaziri nitakaowateua hivi karibuni, ushirikiano mkubwa. Wachangamsheni, lakini watendeeni haki na wapeni ushirikiano.
Mheshimiwa Spika: Nawapongeza Wabunge wote waliochaguliwa. Ninyi, waheshimiwa Wabunge, ndio macho na masikio ya wananchi. Mmeaminiwa na kuheshimiwa. Naomba kila siku mnapoingia au kutoka katika Bunge hili, mnapozungumza humu ndani au mnaposikiliza wengine wakizungumza, mnapokuwa macho au mnapofumba macho kutafakari kwa kina, kila mara mkumbuke imani na heshima hiyo kubwa mliyopewa na wananchi.
Nakupongeza sana wewe mwenyewe, Mheshimiwa Spika, kwanza kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge, na pili kwa kucahguliwa kuwa Spika wa Bunge hili Tukufu. Umepata kazi ya heshima kubwa sana, yenye wajibu mkubwa sana. Unao uwezo na uzoefu wa kuifanya. Hivyo, sina shaka utaimudu vema kazi hiyo, na utaliongoza Bunge hili kwa hekima na busara, ukiwatendea haki Wabunge wote, na upande wa Serikali pia. Ninakutakia kila la kheri, na ninakuhakikishia ushirikiano kamili katika kazi zako.
Mheshimiwa Spika: Ninampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Amani Abeid Karume, kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Zanzibar. Namhakikishia ushirikiano wangu na wa serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Spika: Navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu wakati wote wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu. Wameonyesha uaminifu kwa Taifa na uzalendo wa hali ya juu. Nawapongeza sana.
Mheshimiwa Spika: Wananchi wengi wameelimika na kufuatilia mchakato wote wa Uchaguzi Mkuu kutokana na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na vyombo vya habari. Nawashukuru na kuwapongeza.
Mheshimiwa Spika: Serikali ya Awamu ya Nne ambayo nimepewa heshima ya kuiongoza, inaanza kazi wakati nchi ikiwa na hali nzuri kiuchumi, kisiasa na kijamii. Mafanikio hayo yametokana na uongozi imara na thabiti wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa
Napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa dhati kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanyia nchi yetu. Kwangu binafsi, amekuwa mwalimu na mwelekezi ambaye amenijengea uwezo na dhamira ya kuendeleza kazi aliyoianza. Namtakia afya njema na maisha marefu, yeye, mama Mkapa, na familia yao.
Mheshimiwa Spika: Nazipongeza Tume ya Uchaguzi ya Taifa, na Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kwa kazi nzuri sana waliyoifanya katika chaguzi zilizopita. Naomba waendelee kunoa uwezo wao, maana Watanzania-Bara na Zanzibar wanastahili uchaguzi mzuri. Kadhalika tunao wajibu wa kihistoria wa kuwa mfano bora barani Afrika na hata kwingineko.