Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Guestbook
Tanzania, is a country on the east coast of east Africa.
 
JakayaKikwete.com
 »  Home  »    »  Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
By Mike Mushi | Published  12/30/2005 | | Rating:
MAJUKUMU YA MSINGI YA SERIKALI YA AWAMU YA NNE

Alikarabati na kupanua sana miundombinu ya elimu, afya, maji na umeme. Barabara na madaraja yamejengwa. Kutokana na juhudi za Rais Mkapa, Serikali ya Awamu ya Nne inaanza bila mzigo wa madeni usiobebeka kama alivyoanza yeye. Tunaanzia mahali pazuri.

Mheshimiwa Spika: Ilani ya Uchaguzi wa CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2005 imetamka bayana majukumu mawili ya msingi ya serikali ya Awamu ya Nne.

* Kwanza, kuitoa Tanzania kutoka kwenye dimbwi la uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuiingiza katika mkondo wa uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea.

* Pili, kuwashirikisha wananchi wote kwa njia ya uwezeshaji katika ujenzi wa uchumi na kuutokomeza umasikini.

Mheshimiwa Spika: Kwa kuzingatia majukumu haya ya msingi, na mbinu na mikakati mbalimbali ya kuyatekeleza, Watanzania watarajie mambo kumi yafuatayo katika miaka mitano ijayo:

Kwanza, Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha kuwa Amani, Utulivu na Umoja wa nchi yetu na watu wake vitadumishwa;

Pili, Serikali ya Awamu ya Nne itadumisha na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana tangu serikali ya Awamu ya Kwanza hadi leo;

Tatu, Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza vita dhidi ya umasikini, ujinga na maradhi, tena kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya;

Nne, Serikali ya Awamu ya Nne itatimiza ipasavyo wajibu wake wa utawala na maendeleo, na itaendesha dola kwa misingi ya utawala bora na uwajibikaji; utawala wa sheria unaoheshimu na kulinda haki za binadamu; itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa bila ya woga wala kuoneana muhali.

Tano, Serikali ya Awamu ya Nne itaimarisha uwezo wake wa kulinda maisha na mali za raia wake. Tutapambana na uhalifu wa kila aina, na majambazi hayataachwa yatambe yatakavyo;

Sita, Serikali ya Awamu ya Nne  itahakikisha mipaka ya nchi yetu ipo salama. Hatutamruhusu mtu au nchi yeyote kuchezea mipaka ya nchi yetu na uhuru wetu;

Saba, Serikali ya Awamu ya Nne itafanya kila iwezalo kuhakikisha Tanzania ina mahusiano mazuri na mataifa yote duniani, pamoja na mashirika ya kimataifa na kikanda;

Nane, Serikali ya Awamu ya Nne itajali sana maslahi na mahitaji ya makundi maalum katika jamii kama vile wanawake, vijana, watoto, wazee, walemavu na yatima;

Tisa, Serikali ya Awamu ya Nne itaongoza mapambano mapya na kuhifadhi mazingira ili vizazi vijavyo virithi nchi nzuri, na msingi imara wa maendeleo endelevu; na

Kumi, Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza michezo, na shughuli za utamaduni na burudani.

Comments