SIASA
Mheshimiwa Spika: Chama Cha Mapinduzi kimerejeshwa madarakani kwa kura halali za wananchi zilizotupa idhini ya kutawala, tena idhini kubwa isiyo na shaka hata kidogo. Hatutaona aibu kuitumia idhini hiyo, kupitia Bunge hili, kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005.
Kama mwana-CCM nafurahia sana ushindi wetu. Lakini, nikiwa Rais, napenda niwahakikishie wapinzani kuwa hatuna nia au sera ya kuua vyama vya upinzani. Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza, kwa dhati, mfumo wa siasa wa demokrasia ya vyama vingi. Ushauri wangu kwa vyama vya upinzani kwa wapinzani ni kuwa wasiwe wepesi kutafuta mchawi kila wanaposhindwa uchaguzi. Badala yake nawaomba wajiulize kwa nini Watanzania wamewakataa kiasi hicho. Nina uhakika watapata jibu.
Mheshimiwa Spika: Ni kweli nchi yetu sasa ni ya demokrasia ya vyama vingi. Lakini ni wazi bado utamaduni wa mfumo huu wa siasa ni mchanga na kwa ujumla haujaimarika vya kutosha. Tutajitahidi kujenga utaratibu na misingi ya mahusiano mema zaidi baina ya vyama vya siasa nchini Tanzania. Mimi naamini wakati umefika, kama alivyowahi kusema Rais Mkapa, kuwa tuwe na maadili yatakayotawala shughuli za kisiasa, ambayo hayategemei hiari ya viongozi wa kisiasa waliopo madarakani. Yanakuwa ni maadili na miiko ya lazima, yanayobana kila chama cha siasa, wanachama na viongozi wake, ikiwemo wale wa Chama Tawala. Tusipofanya hivyo na dalili zimeanza kuonekana wanaweza kujitokeza watu wakavuruga nchi yetu kwa kisingizio cha uhuru wa kisiasa. Uhuru bila mipaka ni fujo, na siwezi kukubali nchi miliyonikabidhi kuiongoza itawaliwe na fujo.
Mheshimiwa Spika: Yameanza kujitokeza mawazo kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha. Kama ni kweli, tusipokuwa waangalifu, nchi yetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo. Ni kweli kwamba fedha ni nyenzo mojawapo muhimu katika kufanikisha uchaguzi. Lakini, fedha kutumika kununua ushindi si halali.
Ni vema sasa tuanzishe mjadala wa kitaifa na hatimaye kuelewana kuhusu utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutafuta fedha za uchaguzi; na utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutumia fedha hizo. Na utaratibu tutakaokubaliana uwe ni sehemu ya maadili ya uchaguzi katika uchaguzi wa kiserikali na ndani ya vyama vya siasa. Katika Mjadala huo suala la takrima nalo tuliangalie
MAJUKUMU YA MSINGI YA SERIKALI YA AWAMU YA NNE
Mheshimiwa Spika: Tangu tupate Uhuru, kila awamu ya uongozi wa taifa imekuwa na majukumu yake ya msingi. Awamu ya Kwanza iliunda na kujenga taifa. Wakoloni hawakujenga hisia za utaifa, maana mkakati wao wa kututawala ulikuwa kutudhoofisha kwa kutugawa ili tutawalike kwa urahisi. Mwalimu Nyerere hakurithishwa taifa na wakoloni. Alirithishwa mkusanyiko wa makabila mbalimbali, na watu wa dini na rangi mbalimbali. Akatambua kuwa hata uchumi wa Tanzania ungekua kwa kasi kubwa kiasi gani, iwapo hakuna misingi imara na hisia za dhati za utaifa, baada ya muda tutasambaratika na uchumi huo utakuwa hauna maana..Kwa kushirikiana na hayati Mzee Karume wakatujengea Taifa la Tanzania lenye umoja, pamoja na watu wake kuwa wa makabila 120, rangi na dini mbalimbali.
Mwalimu aliongoza vita dhidi ya ujinga, umasikini na maradhi. Mtandao mkubwa wa huduma za jamii tunaojivunia leo ulianza na falsafa ya maendeleo ya Baba wa Taifa. Wengi wetu tuliomo humu ndani, wa makamo yangu, tusingesoma na kufika hapa tulipo kama si kuona mbali na sera nzuri za Baba wa Taifa. Tutamshukuru yeye na Mzee Karume daima.
Awamu ya Pili chini ya Mzee wetu, Ali Hassan Mwinyi, ilifungua milango na kupanua uwanja wa ushiriki wa wananchi kwenye uchumi na siasa. Mzee Mwinyi ni muasisi wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa Tanzania. Alimaliza uhaba wa bidhaa na baadhi ya huduma muhimu uliodhalilisha wananchi. Alipanua sana mipaka ya uhuru wa raia katika maisha yao ya kiuchumi na kisiasa.
Nakumbuka siku moja Mzee Mwinyi alielezea awamu yake kama wakati ambapo mtu anafungua madirisha ya nyumba ili hewa safi iingie ndani. Lakini, akasema, ukifungua madirisha ujue nzi, mbu na wadudu wengine nao wataingia.
Hapo ndipo Awamu ya Tatu ya Rais aliyenitangulia, Mheshimiwa William Mkapa, ilipoanzia. Ilibidi kushughulikia mbu, nzi na wadudu hao. Rais Mkapa alifanya kazi kubwa kurejesha nidhamu kwenye ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali. Alipiga vita rushwa kwa nguvu zake zote. Alirejesha mahusiano mazuri na wahisani wetu na washirika wetu kwenye maendeleo. Aliweka mazingira bora ya uwekezaji, na ukuaji wa uchumi. Aliimarisha misingi ya uchumi mkuu.Bei za kuruka, na fedha za soksi zikaisha. Ameweka misingi imara ya kuwezesha wananchi kujiendeleza kupitia miradi kama vile TASAF na MKURABITA chini ya mwavuli wa MKUKUTA.