Mheshimiwa Spika: Amani na utulivu wa nchi yetu ni moja ya agenda kubwa ya serikali ya Awamu ya Nne. Maendeleo ya uchumi pia yanategemea sana utulivu wa nchi. Pamoja na matukio ya hapa na pale nchi yetu kwa jumla imetulia, na ni wajibu wetu kuuendeleza utulivu huu, kwa kufanya yafuatayo:
Kwanza, kujenga mazingira mazuri ya kazi kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama;
Pili, kuendeleza juhudi za kuwa na Majeshi ya ulinzi na Usalama yaliyo imara yenye nidhamu ya hali ya juu na utii, na yenye utaalam na zana za kisasa;
Tatu, kuongeza uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama kupambana na ujambazi na kuzagaa kwa silaha ndogondogo ambazo zinatumika kufanyia uhalifu dhidi ya raia wema. Tatizo hili tutalivalia njuga.
Nne, kuanzisha na kutoa vitambulisho vya uraia; na
Tano, kuongeza kasi ya urejeshaji wa wakimbizi makwao.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika: Waheshimiwa Wabunge: Nimesema mengi. Kwa leo inatosha. Ninamalizia kwa kuwahakikishieni kuwa nafahamu vizuri sasa ukubwa wa heshima na uzito wa majukumu niliyokabidhiwa na Watanzania wenzangu. Ninafahamu matarajio ya Chama changu, chama cha Mapinduzi. Nitaongoza kwa dhati utekelezaji wa ahadi zetu kwa wananchi, na kwa dunia. Ninayajua matarajio ya Watanzania wenzangu walipoitikia wito wa ari mpya, nguvu mpya, na kasi mpya. Ninayajua matarajio ya nchi jirani, bara la Afrika na dunia kwa Awamu ya Nne ya Uongozi wa taifa letu. Ninajua wahisani wetu na wawekezaji, wa ndani na nje, wananisikiliza kwa makini, wakitaka kujiridhisha iwapo nitavijaza viatu alivyoniachia Rais wetu mpendwa wa Awamu ya Tatu, Benkamin William Mkapa. Nitajitahidi ingawa ni vikubwa kwangu..
Kwenu nyote, na kwao wote, naahidi kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, na kwa ushirikiano na kwa ushirikiano na Bunge hili na wananchi kwa ujumla, kuwa naweza kutimiza matarajio ya kila mmoja.
Tanzania yenye neema tele inawezekana. Maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana. Kila mmoja wetu atimize wajibu wake.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Ahsanteni kwa kunisikiliza.