Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Guestbook
Tanzania, is a country on the east coast of east Africa.
 
JakayaKikwete.com
 »  Home  »    »  Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
By Mike Mushi | Published  12/30/2005 | | Rating:
MAJI

Mheshimiwa Spika: Tatizo la maji ndicho kilio kikubwa cha Watanzania mijini na vijijini. Ndiyo kero nambari wani. Serikali za awamu zote zimefanya jitihada kubwa kukabiliana na tatizo hilo. Serikali ya Awamu ya Nne inakusudia kulikabili tatizo hili kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.

Ni makusudio yangu kuwa tuwe na Mpango Kabambe wa Maji kwa nchi nzima. Mpango ambao utajumuisha mikakati na mbinu mpya za kutekeleza kwa kasi sera ya Maji na kutatua tatizo la Maji. Aidha, tutakamilisha miradi mikubwa ya ukarabati na upanuzi wa Majisafi na Majitaka Dar es Salaam, na ule wa kupeleka maji katika miji ya Kahama, Shinyanga na vijiji vitakavyopitiwa na bomba kutoka Ziwa Victoria.

AFYA

Mheshimiwa Spika: Serikali ya Awamu ya Tatu imechukua hatua mbalimbali kuboresha sekta ya afya, na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi. Tutaendeleza hatua hizo. Huduma ya afya kwa kina mama na chanjo mbalimbali kwa watoto zitaendelea kutolewa na kuboreshwa zaidi. Tunataka kila mtoto wa Kitanzania apate chanjo zote zinazostahili.

Aidha, tutaimarisha mtandao wa kusambaza dawa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati, pamoja na kuendelea kuongeza bajeti na ununuzi wa dawa na vifaa vya tiba. Ukarabati na ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati utaendelea. Kwa kutambua kuwa kinga ni bora kuliko tiba tutakazania pia elimu ya afya. Mapambano dhidi ya malaria na kifua kikuu yatapewa msukumo maalum.

UKIMWI

Mheshimiwa Spika: Nchi yetu inakabiliwa na tatizo kubwa la UKIMWI. UKIMWI ni janga la kitaifa na dunia kwa ujumla. Janga hili limekuwa likiathiri utendaji na kupunguza nguvukazi ya Taifa. Tutaendeleza jitihada za kuhamasisha na kutoa elimu ya UKIMWI kwa wananchi wote ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anao uelewa sahihi wa janga hili. Aidha, serikali itatenga rasilimali zaidi, na kushirikiana na wadau mbalimbali, kuongeza upatikanaji wa dawa za kurefusha maisha na kupunguza makali kwa watu wengi zaidi walioathirika na UKIMWI.

MAKUNDI MAALUM

Mheshimiwa Spika: Katika jamii yetu yapo makundi maalum ambayo Serikali inao wajibu wa kuwasaidia. Kundi la kwanza ni la watoto yatima. TUnahitaji wadau mbalimbali wake pamoja na kuandaa mipango endelevu ya kuwalea na kuwasaidia watoto hawa. Watoto yatima wanahitaji elimu, lishe bora, huduma za afya, makazi na upendo sawa na watoto wengine wa Kitanzania. Serikali ya Awamu ya Nne inaahidi kuwa yatima watapata elimu na huduma ya afya kwa kusaidiwa na serikali

Mheshimiwa Spika: Kundi jingine maalum ni lile la walemavu. Zipo hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa kuwapa fursa walemavu kutumia vipaji vyao ili kujitegemea. Changamoto kubwa kwetu kama Taifa ni kuwa tuache kuwanyanyapaa na tuwaone kuwa ni binadamu wenzetu. Serikali itachukua hatua za  kuhuisha sera na sheria ili kutoa upendeleo maalum kwa walemavu katika utoaji wa huduma mbalimbali na vile vile katika kuweka mazingira yatakayowapa fursa ya kutekeleza majukumu yao kwa jamii.

Mheshimiwa Spika: Lipo pia kundi la wazee wetu. Wazee ni hazina kubwa ya Taifa lolote. Jamii yeyote iliyostaarabika inalo jukumu la kuwaenzi na kuwatunza wazee, tukianza na wanafamilia na wanajamii wa karibu wa mzee anayehusika. Wasikwerpe jukumu hilo asilimia, na la mila za kiafrika. Serikali itahakikisha kuwa kunakuwepo utaratibu na mipango itakayowawezesha wazee kupata huduma muhimu kwa wepesi zaidi na kwa gharama naduu, kwa kuzingatia taratibu, mila na utamaduni wa jamii zetu.

Mheshimiwa Spika: Serikali itazingatia nafasi ya wanawake katika maendeleo. Tutaongeza, awamu kwa awamu, ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi wa kisiasa, kiutendaji na nafasi nyingine za maamuzi. Kadhalika, tutatekeleza ahadi ya kuwawezesha wanawake kiuchumi.

UTALII

Mheshimiwa Spika: Serikali yangu inakusudia kuendeleza sekta ya utalii ili iongeze mchango wake kwenye pato na maendeleo ya taifa letu. Tunapaswa kuboresha huduma kwa watalii kama vile malazi, chakula, usafiri na bidhaa za kumbukumbu za kuwauzia watalii. Tunapaswa kukaribisha wawekezaji wa ndani na nje watakaojenga hoteli zenye hadhi ya kimataifa kuanzia nyota nne hadi tano. Tunahitaji kujenga miundombinu ya kuwafikisha watalii katika maeneo ya kitalii kwa urahisi.

Comments