Mheshimiwa Spika: Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM tulijiwekea lengo la kuongeza nafasi za ajira milioni moja katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Nafasi hizi za ajira zinatarajiwa kupatikana serikalini na katika sekta binafsi. Upanuzi wa sekta za afya, elimu, kilimo, ujenzi wa nyumba na barabara, usindikaji wa mazao na bidhaa asilia, samaki, na utalii ndilo tumaini kuu la ajira. Aidha, matarajio mengine makubwa ya ajira ni kutoka katika sekta isiyo rasmi, yaani ajira binafsi. Tunasisitiza ahadi yetu ya kuchukua hatua thabiti za kuwasaidia vijana, wanawake na Watanzania kwa jumla kupata mikopo na mitaji ya kuwawezesha kujiajiri. Lengo letu ni kuwa kila raia awe na chanzo cha uhakika cha kipato, na kuibua maeneo mapya ya kuwapatia ajira wananchi wengi zaidi.
Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza pia juhudi za kuhimiza, na kuwezesha, uanzishwaji wa viwanda vidogo, vya kati ya vikubwa kama vile vya nguo na vya kuunganisha bidhaa za matumizi ya nyumbani vyenye uwezo mkubwa wa kutoa nafasi za ajira. Serikali ya Awamu ya Tatu ilibuni mradi uitwao Tanzania Mini-Tiger Plan 2020 ambao kwa kutumia maeneo maalum ya uchumi utaongeza mauzo nje ya nchi, na kuongeza haraka nafasi za ajira. Serikali ya Awamu ya Nne itautekeleza mradi huo kwa ukamilifu.
USHIRIKA
Mheshimiwa Spika: Ushirika ni nguzo muhimu ya kuwawezesha wanyonge kuwa na sauti na hivyo kuweza kupambana na umasikini. Serikali ya Awamu ya Tatu imefanya kazi kubwa na nzuri ya kuunda upya ushirika nchini kwa kuhuisha sera na sheria ili kuweka mazingira yatakayochochea kujengeka kwa vyama huyu vya ushirika vinavyoiongoza itaendeleza juhudu hizo pamoja na kuendelea kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi kujiunga na vyama hivyo.
HUDUMA YA JAMII
Kuendeleza huduma za jamii kama vile elimu, afya, maji na kadhalika itaendelea kuwa kipaumbele cha juu cha Serikali ya Awamu ya Nne.
ELIMU
Mheshimiwa Spika: Kazi kubwa ya kupanua miundombinu ya elimu nchini imefanyika katika miaka kumi iliyopita chini ya serikali ya Awamu ya Tatu. Uandikishaji wa wanafunzi, wa kike na wa kiume, katika ngazi zote za elimu umeongezeka sana. Elimu itakuwa agenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya Nne, ambayo itafanya yafuatayo:-
Kwanza, kuendelea kuandikisha watoto wote wa rika lengwa la kuanza shule;
Pili, kuboresha taaluma ili kuongeza viwango vya kufaulu;
Tatu, kuongeza ajira ya walimu wa elimu ya msingi sekondari;
Nne, kushirikiana na wazazi na wadau wengine wa elimu kujenga vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, maabara na vyoo;
Tano, kuongeza ruzuku inayotolewa hivi sasa kwa ajili gharama za kuendesha shule;
Sita, kuimarisha taasisi za kudhibiti ubora wa elimu inayotolewa;
Saba, kutoa fursa na motisha kwa sekta binafsi, taasisi za dini na mashirika binafsi yanayowezekana katika elimu.
Nane, kuimarisha Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili iweze kutoa mikopo kwa wahitaji wengi zaidi;
Tisa, kujenga angalau chuo kikuu kingine kipya; na
Kumi, kuhakikisha kuwa mafunzo ya ufundi stadi yanaendelezwa na kuimarishwa kama mkakati wa kupambana na tatizo la ajira.
Kumi na Moja, kuboresha maslahi ya walimu katika shule na vyuo hapa nchini.