Mheshimiwa Spika: Serikali nitakayoiunda, pamoja na kuheshimu uhuru wa mahakama, itatimiza ipasavyo wajibu wake na kuimarisha miundombinu ya kutoa haki kwa kuongeza idadi ya watumishi, kuwaendeleza kitaaluma, kukarabati majengo yaliyopo na kujenga mapya, na kupeleka huduma za utoaji haki karibu zaidi ya wananchi.
MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI
Mheshimiwa Spika: Kusimamia vizuri mapato na matumizi ya serikali nayo ni sehemu ya utawala bora. Isitoshe, utekelezaji mzuri wa jukumu hilo ndio unaipa serikali uwezo wa kutekeleza mengine yote inayopaswa au inayokusudia kuyatekeleza. Serikali ya Awamu ya Tatu, chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, iliongeza mapato ya serikali mara tano sambamba na kuweka mfumo mpya na wa kisasa wa kudhibiti matumizi, na kuongeza uwazi katika bajeti ya serikali. Hatutalegeza kamba hata kidogo. Hatutavumilia wanaokwepa kulipa kodi stahiki za Serikali au wabadhirifu wa fedha na mali za umma. Sheria ya Fedha, na Sheria ya Manunuzi ya Umma, lazima zifuatwe. Watakaokiuka wachukuliwe hatua za nidhamu. Wasiorejesha masurufu ya safari nao wasivumiliwe.
KAZI ZA SERIKALI KWENYE UCHUMI WA SOKO
Mheshimiwa Spika: Utawala bora ni pamoja na Serikali kufanya vizuri kazi zake nyingine muhimu katika mazingira ya uchumi wa soko. Jukumu la msingi la Serikali ni kutengeneza mazingira mazuri kwa uchumi kukua na biashara kustawi. Kwa sababu hiyo, Serikali ya Awamu ya Nne itatekeleza mambo manane yafuatayo:
Kwanza, kuweka sera na mazingira bora ya kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi;
Pili, kuweka sera nzuri zinazowezesha ukuaji wa uchumi wa kisasa;
Tatu, kuweka mfumo mzuri wa usimamizi wa mazingira ili kulinda uhai wa binadamu na viumbe hai;
Nne, kuweka mifumo bora ya kusuluhisha haraka migogoro ya kibiashara;
Tano, kuweka utawala mzuri wa sheria na wa haki;
Sita, kuwa na taasisi za kudhibiti na kusimamia viwango vya huduma na bidhaa;
Saba, kuwa na sera nzuri za kifedha ili kuhamasisha uwekezaji na uzalishaji; na
Nane, kutekeleza kwa dhati sera ya uwezeshaji wa wazawa.
UCHUMI ENDELEVU WA KISASA UNAOKUA
Mheshimiwa Spika: Serikali ninayoiongoza itatoa kipaumbele katika kujenga uchumi endelevu, wa kisasa, unaokua. Serikali ya Awamu ya Tatu imefanya kazi kubwa katika eneo hilo, na kutuachia msingi imara ambao sisi tutajenga juu yake. Hatutabomoa msingi huo bali serikali itatumia mafanikio hayo kama nyenzo ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wetu.
Mheshimiwa Spika: Sekta binafsi ndiyo mhimili wa uchumi wa nchi yetu hivi sasa. Serikali ya Awamu ya Tatu imeweka mazingira mazuri ya ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi wa Taifa. Aidha, Serikali ya Awamu ya Tatu imejenga mahusiano mazuri na sekta binafsi ambayo sasa imepewa fursa ya kushirikiana na serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini. Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza kazi hiyo nzuri. Tutajitahidi kuwa karibu na sekta binafsi kwa maslahi ya nchi yetu..