Mheshimiwa Spika: Zipo sababu kwa nini nchi yetu imekuwa, kwa kiwango kikubwa, kisiwa cha amani na utulivu katika bahari iliyotibuka. Mojawapo ya sababu hizo, kama nilivyosema, ni sera ambazo kwa makusudi zilijenga hisia za umoja, na hazikuwabagua wala kuwanyima haki watanzania kwa sababu za dini, rangi, kabila, jinsia au eneo wanakotoka. Nitawatarajia watakaokuwa kwenye Serikali nitakayoiunda wasiwabague wananchi kwa sababu yoyote ile, na wawe watetezi thabiti wa haki za binadamu. Ningependa pia tuwe na maadili na miiko ya kitaifa kuhusu jambo hili.
UTAWALA BORA
Mheshimiwa Spika: Serikali nitakayoiongoza itazingatia na kuendeshwa kwa misingi ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji. Tutaheshimu utawala wa sheria, na tutazingatia na kuheshimu mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili mikuu ya dola, yaani Utawala, Bunge na Mahakama. Tutaheshimu uhuru wa Mahakama na Bunge; tutatimiza ipasavyo wajibu wetu; na tutawezesha mihimili hiyo kufanya kazi zake ipasavyo. Serikali ya Awamu ya Nne itaimarisha utendaji Serikalini na kupambana na maovu katika jamii bila woga wala kuoneana muhali.
RUSHWA
Tutaongeza kasi ya kupambana na rushwa kisayansi kwa kushambulia kiini chake, na kuziba mianya yake. Tutajitahidi kuongeza mishahara na kuboresha maslahi ya watumishi wa umma ili kupunguza vishawishi vya rushwa. Tutaendelea pia kuongeza uwazi katika maamuzi ya serikali hasa katika manunuzi na mikataba. Tunaimarisha uwezo wa kifedha na kiutendaji wa taasisi zilizo mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya rushwa, hususan Taasisi ya Kuzuia Rushwa, Jeshi la Polisi na Mahakama. Lakini yote ni bure iwapo wananchi hawatajitokeza kusaidia vyombo hivyo. Naomba ushirikiano huo kutoka kwa wananchi.
Katika harakati za kupambana na rushwa yapo mambo mawili mengine ambayo tutayaangalia kwa karibu. La kwanza ni mikataba. Tutaangalia upya taratibu za mikataba mbalimbali inayoingiwa na serikali, mashirika ya umma na idara zinazojitegemea kwa nia ya kuongeza uwazi na uwajibikaji. Mikataba ni mwanya mkubwa wa rushwa hasa zile kubwa kubwa za wanaotafuta utajiri.
Kadhalika, hatuna budi kuchukua hatua thabiti za kuzuia watumishi wa umma kutumia nafasi zao kujitajirisha na kujilimbikizia mali. Sisemi kwamba ni haramu mtu kuwa tajiri au kuwa na mali. Ninachosema mimi kuwa ni haramu ni kutumia nafasi yako ya utumishi au uongozi wa umma kujipatia manufaa ya kujitajirisha au kujilimbikizia mali.
Jambo hili ndilo linalokera sana watu kuona mtu ambaye hana chochote lakini miezi michache tu baada ya kupata cheo anakuwa tajiri mkubwa. ona majumba ya fahari, ona madaladala, teksi bubu, anaishi maisha ya kifahari na na kadhalika. Wananchi wanayo haki kuhoji, na wanayo haki kupata majibu. Ndugu zangu, naomba tuwe waadilifu. Tusilaumiane. Nataka Yume ya Maadili ya viongozi isione haya kutuuliza jinsi tulivyozipata mali tunazosema tunazo. Nitawasaidia kujenga uwezo wa kufanya hivyo kama tatizo lenu ni hilo.
UTENDAJI SERIKALINI.
Mheshimiwa Spika: Dhana ya utawala bora ni pana sana; ni zaidi ya vita dhidi ya rushwa. Tutahimiza utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa ustadi, kwa haraka na kwa ufanisi. Tunataka watendaji wa serikali wenyewe wawe waadilifu, na wanaowajibika; wawe na ari, moyo, na msimamo wa dhati kuhusu utumishi wa umma na huduma bora kwa umma. Tabia ya "Njoo kesho" na nenda rudi tuache. Mwalimu alituasa linalowezekana leo lisingoje kesho. Napenda huo uwe moyo wa utendaji Serikalini.
Natambua tatizo na malalamiko ya watumishi wa umma kuhusu mishahara na maslahi yao. Tutaliangalia. Tutalishughulikia. Nakusudia mapema iwezekanavyo niteue Tume ya Kuboresha Maslahi ya Watumishi wa Umma. Naomba niwatahadharishe kutokana na matumaini ya miujiza. Tutafanya kinachowezekana kadri uwezo wa Serikali unavyojengeka.