Mwakilishi Mkazi UNICEF
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
Viongozi wa Serikali
Viongozi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Taasisi mbalimbali
Wadau wetu wakuu ambao ni watoto
Waalikwa, mabibi na mabwana
Assalaam Alaykum,
Awali ya yote napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha hapa tukiwa salama na wenye afya njema. Aidha napenda kutumia fursa hii kukushukuru sana Mwakilishi Mkazi wa UNICEF na Timu yako kwa heshima hii kubwa mliyonipa ya kuzindua Ripoti ya Hali ya Watoto Duniani ya Mwaka 2007.
Ndugu Mwakilishi Mkazi,
Kwa niaba ya washiriki wenzangu wa mkutano huu napenda nikushukuru tena kwa kutuchambulia kwa ufasaha mada zilizopo kwenye ripoti ya ‘Hali ya Watoto Duniani’ ya mwaka ujao wa 2007. Napenda pia kumshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kubainisha juhudi za serikali katika kujenga mazingira yatakayoleta usawa wa kijinsia.
Aidha nampongeza Mkurugenzi Mtendaji wa KIWOHEDE kwa kutumia fursa hii kutueleza mikakati wanayoitumia kama asasi ya kijamii katika kuwajengea akinamama uwezo ambao utasaidia kuwapa watoto wao maisha bora.
Waalikwa mabibi na mabwana,
Nina furaha kubwa kushiriki katika uzinduzi wa ripoti hii ya UNICEF kwa sababu inalenga masuala ambayo yanagusa sana moyo wangu, masuala ya ‘Wanawake na Watoto’. Naweza kusema kuwa sote tulioko hapa, tumeshiriki kwa vile tunaamini masuala haya ya ‘Wanawake na Watoto’ yanagusa kwa kiasi kikubwa shughuli zetu za kila siku.
Nimedokezwa kuwa ripoti hii inazinduliwa wakati UNICEF inasherehekea miaka 60 ya kuhudumia akina mama na watoto duniani. Ninaamini kuwa kwa miaka hii 60 watoto wengi wamefaidika na huduma za UNICEF haswa katika afya, elimu, maji safi na masuala mengine yahusuyo haki zao. Napenda niungane na Jumuiya ya Kimatifa kuwapa hongera UNICEF kwa kutimiza miaka 60 ya kuhudumia jamii na pia kuwatakia mafanikio katika majukumu wanayokabiliana nayo sasa.
Ndugu wageni waalikwa
Kwa muda mrefu, nikiwa mwalimu nimeweza kuwa karibu sana na akina mama na watoto. Kwa uzoefu wangu, naelewa matatizo mengi yanayowakumba akinamama na watoto, hasa watoto wa kike, katika jitihada za kujenga maisha yao na yale ya familia zao kwa ujumla. Ni kutokana na ufahamu huu, nimeamua kutumia muda wangu mwingi kuhamasisha jamii kujenga usawa wa kijinsia kwa kuboresha elimu kwa watoto wa kike na kupambana na UKIMWI ambao ni dhahiri unawaathiri zaidi wanawake.
Ndugu wageni waalikwa,
Leo nitaongelea zaidi elimu. Hii ni kwa sababu naamini elimu ni nyenzo muhimu sana katika kupambana na adui ujinga, unyanyaswaji wa kijinsia na hata kudhibiti maambukizi ya UKIMWI. Elimu ni Ufunguo wa kufuli zote zinazomweka mwanamke katika jumba la umaskini, unyanyaswaji, maradhi na hata kupuuzwa.
Kwa maneno rahisi yanayoweza kueleweka na kila mmoja wetu, naweza kusema kuwa elimu ni ‘chanjo ya kijamii’, ambayo itamlinda mtoto wa kike kutoka kwenye ndoa za utotoni, UKIMWI, ukahaba na ajira za utotoni. Faida ya kumsomesha mtoto wa kike ni kubwa mno na ndiyo ukombozi pekee wa kweli wa mwanamke. Viongozi wengi wanaamini na wameitumia sana kauli mbiu hii katika kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike wakisema; ‘Ukimwelimisha mwanamke umeelimisha jamii,’ nami kwa dhati kabisa naunga mkono kauli mbiu hii.
Natambua kuwa serikali ya Tanzania imejizatiti katika kuhakikisha watoto wote wanapata elimu kwa kufuta ada za shule za msingi. Naipongeza serikali kwa kuona umuhimu huu, kwani kwa muda mrefu ada za shule zilikuwa kikwazo kikubwa kwa watoto kutoka familia masikini. Katika hili, walioathirika zaidi ni watoto wa kike.
Kwa bahati mbaya zaidi, mila na desturi zetu nyingi huko nyuma zilimbagua mwanamke na mtoto wa kike katika elimu. Watoto wa kike ndio waliokuwa wanaachwa nyumbani ili wasaidie kazi za nyumbani. Hata baada ya kuondoa kikwazo kikubwa cha ada, bado tunakabiliwa na mifumo ya kimila na desturi ambayo inazuia watoto wa kike kutumia fursa hii adhimu ya elimu.
Wageni waalikwa,
Katika familia nyingi watoto wa kike bado wameachiwa majukumu ya kuhudumia kaya – wanawajibika kupika, kufanya usafi, kuokota kuni, kuchota maji, kuangalia wagonjwa, na kulea wadogo zao. Majukumu haya huanza wakiwa na umri mdogo sana, na kuendelea kuongezwa kadri wanavyokuwa. Mila hizi huonekana ni njia nzuri ya kumtayarisha mtoto wa kike kuolewa mapema. Imedhihirika kuwa uzito wa majukumu haya umemlemea mtoto wa kike na kumnyima nafasi ya kuzingatia vizuri masomo na hata kukua vizuri kimwili na kiakili. Mbaya zaidi bado tuna idadi kubwa ya wasichana wanaobeba mimba katika umri mdogo na wengine kuozeshwa ndoa za utotoni.
Ndugu wageni waalikwa,
Kazi ya kuleta mabadiliko katika jamii ni kubwa na inayohitaji dhamira ya dhati. Wiki iliyopita nilikuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ambako nilitembelea mashule. Nilisikitika sana kusikia mkoani Lindi, ni asilimia 60 tu ya watoto ndiyo waliweza kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka jana. Asilimia 40 iliyobaki wamekwenda wapi? Sababu zilizotajwa ni pamoja na mimba, kuolewa na hata utoro hasa kwa watoto wa kiume. Sababu hizi zote tunaweza kupambana nazo na watoto wakamaliza shule.
Nimezungumza na viongozi wa serikali, wazazi na hata watoto wenyewe. Kwa kweli tusipobadilika na kulipa umuhimu unaostahili suala la elimu, nchi yetu itaendelea kuwa masikini kwa miaka kadhaa ijayo.
Ndugu zangu, nimefurahi kuwa nanyi wadau wa watoto leo hii. Naomba tuunganishe nguvu zetu kupambana na changamoto zinazotukabili. Tujitahidi kupita vita mila na desturi zote zinazowanyima watoto hasa wa kike fursa ya elimu. Ni dhahiri kuwa mila hizi sio tu zinawanyima watoto nafasi ya kupata elimu, bali pia huwanyima fursa za kujijengea maisha bora kwao na kwa familia zao.
Ni wazi kuwa tukiunganisha nguvu zetu tutazikabili changamoto hizi kwa urahisi zaidi. Tunapaswa kujipanga vema kuhamasisha kuwanzia ngazi ya familia, mashuleni, katika jamii na hata serikalini. Naamini kwamba kila mmoja wetu akitumia nafasi yake kuhamasisha tutafanikiwa. Nawaomba wanasiasa na viongozi wa dini watusaidie. ingawa wadau tuko wengi na tunapambana kwa njia tofauti, lakini wote tuna lengo moja la kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu, na wanabakia shule mpaka watakapohitimu.
Nawapongeza sana UNICEF kwa kuzingatia umuhimu wa kuunganisha huduma za kinamama na watoto. Tumesikia kutoka KIWOHEDE jinsi ambavyo watoto hufaidika pale maisha ya mama zao yanapoboreshwa.
Ndugu wageni waalikwa,
Nawaomba wote tukaisome tena na tena ripoti hii ya ‘Hali ya Watoto Duniani kwa mwaka 2007’, na kutumia mikakati iliyopo kupanga njia bora za kusaidia kuleta usawa wa kijinsia katika jamii zetu. Tuongeze juhudi za kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu na kushirikiana kikamilifu na watoto wa kiume katika kujenga taifa letu.
Mwisho nawashukuru kwa dhati kabisa wageni wenzangu wote wanawake, wanaume, wadau wa elimu, watoto na wanahabari kwa kushiriki majadiliano ya mkutano huu muhimu wa kujadili hali ya watoto.
Baada ya kuyasema hayo, natamka kuwa Ripoti ya Hali ya Watoto Duniani kwa mwaka 2007 sasa imezinduliwa rasmi.
Asanteni Sana kwa kunisikiliza