HOTUBA YA WAZIRI MKUU MHESHIMIWA EDWARD LOWASSA, (MB), WAKATI WA KUWASILISHA TAARIFA YA MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA NNE KUHUSU UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM (2005) JANUARI HADI DESEMBA KWENYE MKUTANO WA HALMASHAURI KUU YA CCM TAREHE 20 - 21 DESEMBA, 2006 DODOMA.
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete,
Mwenyekiti wa CCM Taifa;
Mheshimiwa Aman Abeid Karume,
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Zanzibar;
Mheshimiwa Dkt. Alli Mohamed Shein, Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Yussuf Rajab Makamba,Katibu Mkuu wa CCM;
Mheshimiwa Alli Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa
Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM;
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Manaibu Waziri;
Mabibi na Mabwana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukushukuru sana kwa kunipa heshima kubwa ya kusimama mbele ya Mkutano huu kuwasilisha Taarifa ya Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005 kwa kipindi cha Januari hadi Desemba, 2006.
Tarehe 21 Desemba, 2005 Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Nne wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuapishwa kwake ni matokeo ya ushindi wa kishindo wa Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu nchini uliofanyika tarehe 14 Desemba, 2005. Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alishinda kwa asilimia 80.28 ya kura zote zilizopigwa. Matokeo ya Uchaguzi Mkuu yalionyesha mapenzi makubwa waliyonayo wananchi kwa CCM. Matarajio na matumaini yao kwa Serikali yako Ndugu Mwenyekiti ni makubwa sana.
Ndugu Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Nne iliingia madarakani kutekeleza dhamira na lengo kuu la Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005 ya chama chetu la kuwezesha kupatikana kwa Maisha Bora kwa kila Mtanzania.
Katika Ilani hiyo, Chama Cha Mapinduzi kimetamka majukumu yake mawili ya msingi yatakayotoa dira kwa Serikali zake kuwa ni:
- Kuitoa Tanzania kutoka kwenye dimbwi la uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuliingiza katikamkondo wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea; na
- Kuwashirikisha wananchi wote kwa njia ya uwezeshaji katika ujenzi wa uchumi na kuutokomeza umaskini.
Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe, kazi zilizotekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Nne zimelenga katika kuweka msingi imara wa kutuwezesha kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye majukumu hayo mawili makubwa.
Alipolihutubia Taifa tarehe 30 Desemba, 2005 wakati wa hotuba ya Uzinduzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alieleza jinsi Serikali anayoiongoza itakavyotekeleza ahadi zilizotolewa na Chama Cha Mapinduzi kwa wananchi. Ili kutoa dira ya kazi za Serikali, Mheshimiwa Rais alibainisha maeneo yatakayopewa kipaumbele na Serikali yake katika kipindi cha miaka mitano ijayo kama ifuatavyo:
- Kuhakikisha kuwa amani, utulivu na umoja wa nchi yetu na watu wake vinadumishwa;
- Kudumisha na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi leo;
- Kuendeleza vita dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi, tena kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.
- Kutimiza ipasavyo wajibu wake wa utawala na maendeleo na kuendesha dola kwa misingi ya utawala bora na uwajibikaji, utawala wa sheria unaoheshimu na kulinda haki za binadamu;
- Kuimarisha uwezo wake wa kulinda maisha na mali za raia wake. Kupambana na uhalifu wa kila aina na kwamba majambazi hayataachwa yatambe yatakavyo;
- Kuhakikisha mipaka ya nchi yetu ipo salama. Kutomruhusu mtu au nchi ye yote kuchezea mipaka ya nchi yetu na uhuru wetu;
- Kufanya kila iwezalo kuhakikisha Tanzania ina mahusiano mazuri na mataifa yote duniani pamoja na Mashirika ya Kimataifa na Kikanda;
- Kujali sana maslahi na mahitaji ya makundi maalum katika jamii kama vile wanawake, vijana, watoto, wazee, walemavu na yatima;
- Kuongoza mapambano mapya ya kuhifadhi mazingira ili vizazi vijavyo virithi nchi nzuri na misingi imara ya maendeleo endelevu;
- Kuendeleza michezo na shughuli za utamaduni na burudani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya mafanikio ya mwaka mmoja ninayoiwasilisha mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, inaeleza kwa muhtasari kazi zilizotekelezwa na Serikali na ambazo zimetuwezesha kupata mafanikio hayo. Wajumbe wamepewa taarifa ndefu yenye maelezo ya kina kwa sekta zote. Kwa msingi huo nitawasilisha taarifa hiyo kwa kueleza kwa muhtasari tu mafanikio ya baadhi ya sekta.
Ulinzi na Usalama
Ndugu Mwenyekiti, katika muda wa mwaka mmoja Serikali ya Awamu ya Nne ilichukua hatua madhubuti kushughulikia hali ya ujambazi iliyokuwa inaanza kutishia amani na utulivu nchini.
Serikali ilipanga upya safu za uongozi wa Jeshi la Polisi na kuliongezea uwezo wa kiutendaji. Kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya ujambazi. Tumefanikiwa kuendeleza na kuimarisha umoja wetu. Wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tatu wa Chama Cha Mapinduzi, Oktoba, 22 1987, Dodoma, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alisema:
“Tukiulizwa na wenye kiburi na fidhuli ya wingi wa mali: Mna nini ninyi Watanzania? Tunaweza kujibu, si kwa fidhuli, lakini kwa fahari kabisa, tuna umoja na amani, vitu ambavyo havinunuliki kwa kiasi chochote cha fedha”.
Moja ya fahari kubwa na ya kujivunia ya Serikali ya Awamu ya Nne ni kuweza kuendeleza hali hii na kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya ujambazi. Mipaka yote ya nchi yetu na nchi jirani ni shwari. Aidha, kurejea kwa amani kwenye nchi za Burundi na DRC kumewezesha wakimbizi 62,499 kurejea makwao na hivyo kutupunguzia mzigo.
Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali
Ndugu Mwenyekiti, hali ya mapato ya Serikali imeendelea kuwa ya kuridhisha. Mamlaka ya Mapato Tanzania imeendelea kupanua wigo wa mapato na hivyo kuweza kuwafikia walipa kodi wengi zaidi. Mapato ya ndani kwa robo mwaka Julai hadi Septemba, 2006 yalikuwa shilingi milioni 634.917. Lengo la kipindi hicho lilikuwa kukusanya shilingi milioni 596,303. Hivyo Mamlaka imevuka lengo la makusanyo kwa asilimia 6.5. Aidha, Mamlaka imeweza kufikia kiwango cha juu cha ukusanyaji wa mapato mwezi Septemba, 2006 ambapo mapato ya Serikali yalifikia shilingi bilioni 231.9.
Makusanyo ya miezi mingine ya mwaka wa fedha 2006/2007 vilevile yalivuka malengo yaliyowekwa. Makusanyo kwa kila mwezi yalikuwa kama ifuatavyo:
Julai, shilingi bilioni 170.01;
Agosti shilingi bilioni 192.09;
Oktoba shilingi bilioni 190.95; na
Novemba shilingi bilioni 195.91.
Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira
Ndugu Mwenyekiti, Serikali imeendelea kusimamia programu mbalimbali zenye lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi ili mchango wao katika ukuaji wa uchumi kitaifa uongezeke. Programu hizo ni pamoja na:
- Uwezeshaji wananchi kiuchumi;
- Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, TASAF;
- Mkakati wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA);
- Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA);
- Mpango Maalumu wa Kuharakisha Maendeleo 2020.
Ndugu Mwenyekiti, katika juhudi za Serikali za kuwawezesha wananchi kiuchumi, jumla ya shilingi bilioni 21 zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2006/2007 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wananchi wakiwemo vikundi vya wajasiria mali au mtu mmoja mmoja Tanzania Bara. Hadi Desemba, 2006 kiasi cha shilingi bilioni 10.5 zilikuwa zimepelekwa Benki za CRDB na NMB ili ziweze kukopeshwa kwa wananchi kwenye matawi yao ya mikoani. Kiasi kilichobaki kitakopeshwa kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali yatakayoainishwa baadaye. Taratibu zingine za kufanikisha zoezi hili zinaendelea kuandaliwa ikiwa ni pamoja na mafunzo kwa wataalam watakaohusika na mchakato wa kutoa mikopo.
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
Katika kipindi cha Januari - Desemba 2006, TASAF ilishughulikia jumla ya maombi ya miradi 1,589 kutoka Halmashauri mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar. Kati ya maombi hayo; 1,262 ni miradi ya huduma za jamii, 126 ni miradi ya kaya zenye uhaba wa chakula na miradi 201 ni ya makundi maalum. Utekelezaji wa miradi hiyo uligawanywa kwa makundi yote matatu ya walengwa kama ifuatavyo: Miradi ya elimu 768, maji 216, afya 193, barabara 153, chakula 88, masoko 52, mifugo 44, ustawi wa jamii 39, misitu 22, uvuvi 5, umwagiliaji maji mashamba 4, ushirika 2 na mazingira 1. Miradi yote hiyo ina thamani ya shilingi 49,775,420,390.
Mkakati wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania
Ndugu Mwenyekiti, Serikali imebuni utaratibu wa kuzipa uhai kisheria ardhi na nyumba ambazo miaka ya nyuma hazikutambuliwa kisheria kama dhamana ya kupata mikopo katika vyombo vya fedha. Katika muda wa mwaka mmoja nyumba 220,000 kati ya 400,000 zimetambuliwa katika Jiji la Dar es Salaam na kati ya hizo wamiliki wa nyumba 45,000 wamepatiwa leseni za makazi ambazo ni hati zinazotambuliwa kisheria. Utekelezaji wa mkakati huu unaendelea pembezoni mwa Jiji na kuangalia uwekaji wa huduma muhimu za makazi kama shule, hospitali, na masoko.
HUDUMA ZA UZALISHAJI MALI
Kilimo
Ndugu Mwenyekiti, Serikali ilikamilisha maandalizi na kuzindua Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo ya miaka saba (2006/2007 – 2012/2013). Programu hii ambayo itagharimu shilingi trillion 2.5 ni matokeo ya ushirikiano baina ya wadau mbalimbali na Serikali. Ushirikiano wa aina hii umetuwezesha kuanzisha Mfuko ambao utawezesha utekelezaji wa programu hii.
Aidha, Serikali vilevile imeimarisha usambazaji wa mbolea na mbegu bora kwa kuongeza fedha za ruzuku ya mbolea toka shilingi bilioni 7.0 (mwaka 2005/06) hadi shilingi bilioni 21.0 mwaka 2006/07. Hadi Desemba, 2006 tani 92,543.32 za mbolea na tani 325.5 za mbegu zenye ruzuku zimepokelewa kwenye vituo vya mikoani vya usambazaji. Aidha, pembejeo na zana za kilimo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.32 zimetolewa na kusambazwa kwa wakulima.
Ili kukabiliana na upungufu wa chakula uliokuwa umejitokeza nchini jumla ya tani 99,676 za chakula zilitolewa kusaidia watu 564,723 ambao hawakuwa na uwezo wa kununua chakula cha bei nafuu. Serikali ilitoa tani 122,638 za mahindi kwa walioathirika na upungufu wa chakula zikiwemo tani 15,537 zilizotolewa bure.Ili kuimarisha Hifadhi ya Taifa ya Chakula hadi Desemba 2006 Serikali imetoa kiasi cha Tshs.21,282,596,833 kilichowezesha jumla ya tani 104,014 za mahindi na tani 2,252 za mtama kununuliwa na kusafirishwa.
Wananchi wa mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wameitikia kwa ari kubwa uimarishaji wa kilimo cha korosho. Katika msimu huu inatarajiwa uzalishaji kufikia tani 110,000. Juhudi hizi za wakulima hata hivyo zimekumbana na matatizo ya ununuzi wa korosho. Akiwa katika ziara ya mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kuhusu ununuzi wa korosho yote ya wakulima na kwamba makampuni yaliyopewa leseni kufanya hivyo yatimize wajibu wao. Hadi hivi sasa asilimia 60 ya korosho imeshanunuliwa. Serikali imehimiza makampuni yanayonunua korosho yaelekeze nguvu katika maeneo ambayo bado korosho haijanunuliwa kwa wingi ambayo ni Wilaya za Tunduru, Liwale, Masasi, Mtwara Vijijini, Rufiji, Mkuranga, Kibaha na Kisarawe. Aidha, Serikali imewachukulia hatua kwa kuwafutia leseni makampuni 7 yaliyoshindwa kutimiza wajibu wao wa kununua korosho. Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu ununuzi wa korosho ili kuwawezesha wananchi kuuza korosho yote waliyonayo. Hata hivyo suluhisho la matatizo haya ya ununuzi wa mazao ya wakulima ni kuwa na vyama vya ushirika vyenye nguvu.
Maendeleo ya Ushirika
Ushirika wenye nguvu ndio kichocheo cha kujengeka kwa kundi kubwa la wajasiriamali mijini na vijijini. Aidha, ushirika wenye nguvu utakuwa vilevile kichocheo cha kilimo chenye tija. Serikali imechukua hatua maalum za kuhamasisha uanzishwaji wa Vyama vya Akiba na Kukopa (SACCOS). Hadi tarehe 30 Novemba, 2006 jumla ya SACCOS mpya 901 zilikuwa zimeanzishwa na kusajiliwa. Kusajiliwa kwa vyama hivyo, kumeongeza idadi ya SACCOS zilizosajiliwa nchini kufikia 2,776 zikiwa na wanachama 384,806.
Uzalishaji Viwandani
Ndugu Mwenyekiti, ili kuendeleza wazalishaji na wafanyabiashara wadogo, Serikali imeweka msukumo katika uanzishaji wa mifuko ya kuwawezesha kuhimili ushindani. Mfuko wa wafanyabiashara wananchi (NEDF) ulipewa Sh. Bilioni 1.0 kuwasaidia wajasiriamali kupitia umoja huo, kupata mikopo midogo midogo. Aidha, Mfuko wa kudhamini mikopo ya wajasiriamali wadogo umeanzishwa kwa mtaji wa Sh. Bilion 2.0. Taratibu za kutumia fedha hizo zimekamilika na Benki 16 zimeonyesha utayari wa kushiriki katika programu hiyo.
Nishati na Madini
Ndugu Mwenyekiti, kazi kubwa iliyofanyika katika sekta ya madini ni pamoja na kuendelea kuvutia wawekezaji, kupitia mikataba iliyopo ya madini na kuanzisha mazungumzo na wawekezaji wakubwa wa madini namna ya kuweza kufaidika zaidi kama Taifa kutokana na madini yetu. Lengo ni kuwa na makubaliano yenye manufaa kwa pande zote – wawekezaji na Serikali. Kampuni ya Barrick inayomiliki migodi ya Bulyanhulu, North Mara, Tulawaka na kampuni ya Resolute inayomiliki mgodi wa Golden Pride zimefikia makubaliano na Serikali. Moja ya makubaliano hayo yalihusu Halmashauri sita za wilaya ya Tarime, Kahama, Nzega, Biharamulo na Geita kupata Dola za Kimarekani 200,000 (sawa na Tshs. 252,000,000) kila Halmashauri kwa mwaka kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Aidha, kutokana na makubaliano hayo ambayo yaliongozwa na Rais mwenyewe, Serikali inategemea kupata sio chini ya shilingi bilioni 10 kutoka kwa wawekezaji hawa. Nakupongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hiyo nzuri sana.
Nishati
Mitambo iliyoko kwenye Gridi ya Taifa ina uwezo wa kuzalisha megawati 850. Mitambo inayotumia nguvu za maji ina uwezo wa kuzalisha megawati 560 ikiwa ni asilimia 66 ya umeme wote kwenye Gridi ya Taifa. Kiasi kilichobaki cha megawati 290 kinazalishwa na mitambo inayotumia mafuta au gesi asilia.
Hali ya ukame iliyoikumba nchi yetu kuanzia mwaka 2003 imeathiri sana hali ya maji kwenye mabwawa yanayotumika kwa ajili ya uzalishaji wa umeme. Hali hiyo ilisababisha upungufu wa megawati 450 kutoka katika vyanzo hivyo vya nguvu za maji. Kwa mfano,
- Uzalishaji katika kituo cha Kidatu ulipungua kutoka megawati 204 hadi kufikia megawati 10 na hivyo kupoteza megawati 194.
- Mtera ilifungwa kabisa na hivyo kupoteza megawati 80.
- Kihansi ilifungwa nyakati za asubuhi kuruhusu bwawa lijae na kuzalisha megawati 30 nyakati za jioni na hivyo kupoteza megawati 180 asubuhi na megawati 150 jioni.
Serikali ilichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuwezesha kuongezeka kwa umeme unaozalishwa kutokana na gesi asilia. Hivi sasa mitambo ya SONGAS inazalisha karibu megawati 172. Kampuni ya Aggreko inazalisha wastani wa megawati 40. Kampuni ya Richmond itaingiza kwenye gridi megawati 100. Wanatarajia kuingiza katika gridi ya Taifa megawati 20 za mwanzo wakati wowote kuanzia hivi sasa. Aidha, kutokana na kubadilika kwa hali ya mvua katika nyanda za juu za nchi yetu kumekuwepo na ongezeko la uzalishaji wa umeme.
- Hale inazalisha megawati 9.8.
- New Pangani Falls inazalisha megawati 68
(full capacity)
- Nyumba ya Mungu inazalisha megawati 3.5.
- Kidatu inazalisha megawati 156 nyakati za usiku.
- Kihansi megawati 166 nyakati za usiku.
Ndugu Mwenyekiti, Serikali inaendelea kupanua wigo wa vyanzo vya umeme ili kukidhi mahitaji ya umeme nchini kwa matumizi ya viwandani na majumbani. Moja ya kazi nzuri ambayo karibu itakamilika ni kuhakikisha kwamba mikoa ya Lindi na Mtwara inapatiwa umeme wa uhakika kutokana na gesi asilia kutoka Mnazi Bay. Kazi za ufungaji wa mashine za kuzalisha umeme wa Megawati 12 kwa ajili ya mikoa ya Mtwara na Lindi karibu zitakamilishwa ili kuwapa wananchi wa mikoa hiyo umeme wa uhakika.
Maendeleo ya Ardhi
Ndugu Mwenyekiti, Serikali imepima jumla ya viwanja 8,000 nchini kote na jumla ya Hati 4,241 zimesajiliwa na kutolewa kwa wamiliki mbalimbali wa ardhi. Hadi Novemba, 2006, upimaji wa mipaka ya vijiji 252 ulikuwa umekamilika kama ifuatayo; Bagamoyo (83), Kisarawe (20) Chunya (75) na Kibaha (24). Vyeti vya vijiji 279 vimetolewa na hatimiliki za kimila 1,474 zilitayarishwa, kusajiliwa na kutolewa kwa wenye mashamba. Masjala za Vijiji 11 kati ya 1,100 zimeanzishwa, Masijala 3 za Wilaya ya Handeni, Kilindi na Babati zimejengwa na kupatiwa samani na vitendea kazi, ili ziwe na kumbukumbu sahihi za wamiliki wa viwanja na mashamba na kurahisisha upatikanaji wa hatimiliki za ardhi.
Barabara
Ndugu Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka mmoja, Serikali ya Awamu ya Nne imejenga jumla ya kilometa 257.8 za barabara za lami na kilometa 153.5 za changarawe katika sehemu mbalimbali nchini. Aidha, kilometa 26.8 za barabara za lami na kilometa 890 za changarawe zimefanyiwa ukarabati mkubwa. Vilevile Serikali imefanya matengenezo ya kawaida ya barabara za lami zenye urefu wa kilometa 2,716 na barabara za changarawe zenye urefu wa kilometa 2,523. Kwa upande wa madaraja, Serikali imejenga madaraja 16 na kukarabati madaraja 606.
Huduma za Jamii
Ndugu Mwenyekiti, huduma za jamii kama zilivyoainishwa katika Ilani ni rasilimali watu walioelimika, wenye afya na wenye huduma ya maji safi. Kipaumbele kimewekwa katika kuwapatia wananchi elimu bora, huduma bora za afya na maji safi.
Elimu ya Msingi
Ndugu Mwenyekiti, jumla ya wanafunzi katika shule za msingi imeongezeka kutoka 7,541,208 mwaka 2005 hadi 7,959,884 mwaka 2006 ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.1. Aidha, ujenzi wa madarasa mapya 4,677 umekamilika, vyoo 9,362 vilijengwa na nyumba za walimu 4,504 zilikamilika. Katika kuboresha kiwango cha ubora wa elimu, uwiano wa mwanafunzi kwa mwalimu katika darasa umefikia 1:52 mwaka 2006 ikilinganishwa na 1:55 mwaka 2005. Aidha, walimu 21,578 wa Daraja la B na C walifanya mtihani mwaka 2006 kwenda Daraja A na asilimia 88 walifaulu.
Elimu ya Sekondari
Ndugu Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka mmoja, tumefanikiwa kuwahimiza wananchi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kwamba wanafunzi zaidi waliofaulu darasa la saba wanajiunga na kidato cha kwanza. Katika kipindi cha Januari – Desemba 2006 jumla ya madarasa mapya 1,569 na nyumba za walimu 908 zilikamilika. Aidha, shule mpya 489 zimefunguliwa. Jumla ya wanafunzi 229,000 sawa na asilimia 75.1 ya waliofaulu waliweza kujiunga na kidato cha kwanza.
Ndugu Mwenyekiti, idadi ya wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba imeongezeka kutoka wanafunzi 304,938 mwaka 2005 hadi kufikia wanafunzi 468,187 mwaka 2006. Matokeo haya ni ongezeko la kutoka asilimia 61.7 ya wanafunzi waliofaulu mwaka 2005 hadi asilimia 70.5 mwaka 2006. Inatarajiwa kwamba kila mkoa utapeleka asilimia isiyopungua 70 ya wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza ifikapo mwezi Januari, 2007. Msisitizo umewekwa katika kujenga vyumba zaidi vya madarasa na shule zaidi ili asilimia kubwa ya wanafunzi waliofaulu waweze kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari.
Maji
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Nne imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji nchini (Rural Water Supply and Sanitation program). Mradi huo unatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kati ya mwaka 2006/07 na 2010/11. Gharama za kutekeleza mradi huo ni mchango wa shilingi bilioni 290 kutoka kwa Wabia wa Maendeleo na shilingi bilioni 26 zitakazotolewa na Serikali. Maandalizi ya mradi katika wilaya mbalimbali nchini kupitia wahandisi waelekezi yamefikia hatua nzuri.
Vilevile, maendeleo ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Kahama na Shinyanga, ni mazuri. Kati ya shilingi bilioni 52.2 zilizotengwa katika mwaka 2006/07, karibu shilingi bilioni 43.2 zimekwishatumika. Kazi kubwa zilizofanywa ni pamoja na kujenga tanki la maji sehemu ya Mabale, kujenga mitambo ya kuchuja na kusafisha maji eneo la Ihelela na kulaza mabomba ya maji ambayo hivi sasa yanakaribia kufika Shinyanga mjini.
Mambo ya Nje na Ushirikiano Kimataifa
Ndugu Mwenyekiti, ili kuipa msukumo Sera ya Diplomasia ya Uchumi, wewe mwenyewe umeongoza viongozi, watendaji mbalimbali wa Serikali na wafanyabiashara kufanya ziara na kushiriki katika semina, warsha za kitaifa na kimataifa kwa lengo la kuitangaza Tanzania na kushawishi wawekezaji kuwekeza nchini. Baadhi ya nchi zilizotembelewa ni pamoja na Marekani, Uingereza, Falme za Kiarabu, Japan, Korea ya Kusini, Moscow na China. Kufuatia ziara hizo Kampuni mbalimbali za nje zimeshaanza kuwasili nchini kuangalia uwezekano kuwekeza na kufanya biashara moja kwa moja na Watanzania. Napenda kukupongeza sana wewe mwenyewe kwa kufanikisha sana ziara hizo.
Nchi yetu imeshiriki katika kufanikisha upanuzi wa Jumuiya uliowezesha Rwanda na Burundi kuwa wanachama. Kupanuka kwa jumuiya hii kuna faida kubwa kwa nchi yetu kiuchumi na kibiashara.
MASUALA MTAMBUKA
Mazingira
Ndugu Mwenyekiti, Serikali ya awamu ya nne katika harakati za kuhifadhi mazingira chini ya Makamu wa Rais Dkt. Mohamed Shein, imeanza kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Hifadhi ya Mazingira ya mwaka 2004. Aidha, imeandaa na kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kuhifadhi mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji kuanzia Machi, 2006. Wafugaji waliovamia bonde la Usangu hasa maeneo ya Ihefu na vyanzo vingine vya maji wameondolewa wote kwa operesheni maalum. Zaidi ya ng’ombe 431,774 na mifugo mingine 9,911 imepatiwa vibali vya kuondoka Wilayani Mbarali. Hali ya Bonde la Ihefu imeanza kurejea katika hali yake ya kawaida na wanyamapori na maji yameongezeka kwa kiasi kikubwa.
Mapambano Dhidi Ukimwi
Ndugu Mwenyekiti, Serikali imeongeza juhudi za kutafuta rasilimali kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI. Fedha dhidi ya UKIMWI zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 295 mwaka 2005/2006 hadi shilingi bilioni 567 mwaka 2006/2007. Katika kipindi hicho fedha kutoka Serikalini zimeongezeka kutoka Shilingi bilioni 35 hadi bilioni 88 Wahisani nao wameongeza mchango wao kutoka Shilingi bilioni 260 mwaka 2005/2006 hadi 391 mwaka 2006/2007.
Ndugu Mwenyekiti, upatikanaji wa dawa za kurefusha maisha umeleta ahueni na matumaini kwa waishio na virusi vya UKIMWI. Hivi sasa zaidi ya wagonjwa 54,000 wanapata dawa hizo katika hospitali 200. Aidha wagonjwa wengine wapatao 60,000 wamefanyiwa tathimini na wanaweza kuanza kutumia dawa wakati wowote. Kuna zaidi ya vituo 1000 vinavyotoa huduma ya ushauri na upimaji wa hiari, na vituo 660 vinavyotoa huduma za kudumu za kuzuia maambukizo ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Jitihada za kufikisha huduma hii karibu zaidi na wananchi zinaendelea.
Maendeleo ya Michezo
Serikali imeendelea kutimiza wajibu wake katika kuwezesha kukamilika kwa ujenzi wa Uwanja wa Kisasa Jijini Dar es Salaam. Uwanja huo unategemea kukabidhiwa kwa Serikali mwezi Aprili, 2007. Kwa kuelewa mapenzi makubwa waliyo nayo Watanzania kwa mchezo wa mpira wa miguu, Mheshimiwa Rais amewezesha kuajiriwa kwa kocha wa Timu ya Taifa kutoka Brazil. Hivi sasa wananchi wameanza kuwa na matumaini na timu hiyo baada ya kuona kiwango cha mchezo kimepanda. Kutokana na kuweza kushinda katika michezo ya kimataifa ya hivi karibuni Tanzania sasa imechukua nafasi ya 120 ya viwango vya ubora wa FIFA toka nafasi ya 165 iliyokuwa mwanzo wa mwaka 2006. Kuhusu michezo ya riadha iliyofanyika mwezi Machi huko Melbourne Australia, Tanzania ilipata medali moja ya dhahabu na moja ya shaba na hivyo kushika nafasi ya 17 kati ya nchi 71 zilizoshiriki.
Changamoto Zinazotukabili
Ndugu Mwenyekiti, pamoja na kupatikana kwa mafanikio yaliyoelezwa katika taarifa hii, kumekuwa na changamoto nyingi. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na kukabiliana na matatizo ya upungufu wa chakula uliojitokeza mwanzoni mwa mwaka, umeme wa kutosha na wa uhakika kwa matumizi ya viwandani na majumbani, uharibifu wa mazingira hususan hifadhi vya vyanzo vya maji, kuongeza nafasi katika shule za Sekondari na kuongeza mapato ya Serikali ili kutuwezesha kukabiliana na mahitaji makubwa ya rasilimali. Serikali ya Awamu ya Nne inazitambua changamoto hizo na imedhamiria kuzitafutia ufumbuzi wa haraka katika kipindi cha miaka minne ijayo.
Mwisho
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Nne imeonyesha kwa vitendo uwezo wake wa kutekeleza majukumu yaliyo mbele yetu na ambayo ni ahadi za chama chetu. Ulitoa ahadi kwa Watanzania tarehe 21 Desemba, 2005 kuwa:
“Serikali ya Awamu ya Nne ni ya kujenga juu ya yaliyofanywa na awamu zilizotangulia na kuendeleza yote mema kulingana na mahitaji ya dunia ya leo yenye heri kwa Taifa letu, na kwa dunia yetu, tena kwa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya”
Pamoja na changamoto kubwa zinazotukabili, tunao uwezo wa kutekeleza ahadi za chama chetu kwa wananchi. Mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja yanatudhihirishia hivyo. Katika wosia wake kwa Chama Cha Mapinduzi, Agosti 16, 1990 alipokuwa anang’atuka Uwenyekiti wa CCM Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Nyerere alisema:
"Lazima chama (kijiunde) katika namna ambayo shida, matarajio na mawazo ya wananchi wakati wote yanafikishwa mbele ya Serikali, na vilevile kiweze kuwaeleza wananchi mafanikio, matatizo, mapendekezo na maamuzi ya Serikali."
Ni matarajio ya Serikali kuwa uongozi wa chama katika ngazi zote utaungana na ule wa Serikali katika kufanya kazi ya kuelezea mafanikio haya na kujenga mshikamano wa mawazo na vitendo katika kuendelea kutekeleza ahadi zetu kwa wananchi.
Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe, nawaomba kuwasilisha taarifa hii ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.