HOTUBA YA RAIS WA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
KWENYE KILELE CHA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI, MWANZA, MEI MOSI 2007
Ndugu Rais wa Shirikisho la Vyama
vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA),
Ndugu Johari Juma;
Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo
ya Vijana,
Mheshimiwa John Chiligati;
Waziri wa Kazi, Maendeleo ya
Vijana, Wanawake na Watoto wa
Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar,
Mheshimiwa Asha Abdallah Juma;
Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge;
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza;
Mheshimiwa Getruda Mongela, Rais
wa Bunge la Afrika;
Mama Maria Ducci, Mwakilishi wa
Mkurugenzi Mkuu ILO;
Mama Regina Njaku ¨C Mkurugenzi wa
ILO Kanda ya Afrika;
Mwakilishi wa Shirika la Kazi
Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashairiki,
Mheshimiwa Jurgen
Schwettmann;
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha
Waajiri (ATE),
Dkt. Aggrey Mlimuka;
Waheshimiwa Mabalozi: Balozi wa
Cuba na Balozi wa Uganda ;
Wawakilishi wa Vyama vya Siasa na
Serikali;
Ndugu Wafanyakazi na wananchi
Wenzangu;
Mabibi na Mabwana:
Ndugu Wafanyakazi;
Naomba nianze
kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujalia uhai na afya njema mambo
ambayo yametuwezesha kukutana leo katika sherehe za mwaka huu za Siku ya
Wafanyakazi Duniani tunazoziadhimisha hapa jijini Mwanza. Ni wajibu
kushukuru, kwani kuna baadhi ya wenzetu kwa sababu ya matatizo ya kiafya
wanashindwa kujumuika nasi.
Kadhalika wako
wenzetu hawapo nasi kwa sababu wametangulia mbele za haki. Miongoni mwa
wenzetu hao ni Ndugu yetu mpendwa Faustin Musita aliyekuwa Mwenyekiti wa
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa aliyetutoka tarehe 24 Aprili,
2007.
Napenda
kutumia nafasi hii kuwapeni pole wananchi wenzetu wa Mwanza na
wafanyakazi wote nchini kwa msiba mkubwa huu uliotupata sote. Kifo cha
Musita ambaye pia alikuwa Mratibu wa sherehe hizi za Mei Mosi
hapa Mwanza ni pigo
kubwa siyo tu kwa jumuia ya wafanyakazi nchini, bali pia kwa taifa letu
kwa jumla.
Mimi binafsi
nilimfahamu marehemu kwa kipindi kirefu. Alikuwa mjumbe mwenzangu wa
Kamati ya Utekelezaji ya kwanza ya Umoja wa Vijana wa CCM (1978 ¨C
1984). Ndugu Musita alikuwa mchapa kazi hodari na mzalendo wa hali ya
juu. Alikuwa mtu muwazi na msema kweli asiyeogopa, hivyo sikushangaa
alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za
Mitaa. Marehemu alitumia muda wake mwingi hapa duniani kuwahudumia na
kuwatumikia wanadamu wenziwe kwa moyo na nguvu zake.
Aidha, alikuwa
kiongozi shupavu wa wafanyakazi aliyetetea maslahi yao kwa ujasiri na
bila kuchoka. Ni dhahiri kifo chake kimeacha pengo kubwa siyo tu kwa
familia yake, bali pia kwa nchi yetu kwa ujumla. Tunamwomba Mwenyezi
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amin.
Nawashukuru sana
Viongozi wa Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania kwa heshima hii kubwa
mliyonipa ya kuwa Mgeni Rasmi kwenye sherehe hizi kwa mara ya pili
mfululizo.
Nawashukuruni
pia viongozi na wananchi wa mkoa wa Mwanza kwa mapokezi yenu mazuri na
makubwa yaliyojaa upendo tele. Mimi siwashangai kwani wenyeji wa mkoa
huu mnayo sifa kubwa ya ukarimu na upendo kwa wageni. Tunachokishuhudia
leo ndiyo ukweli wa sifa yenu hiyo.
Napenda
niwapongeze pia viongozi na wananchi wa mkoa huu chini ya uongozi wa
Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa James Msekela, kwa kazi kubwa na nzuri
mliyoifanya ya kuandaa sherehe hizi. Natambua uzito na ugumu wa mzigo
mliobebesywa lakini kwa ushirikiano mzuri baina yenu na wawakilishi wa
wafanyakazi pamoja na Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana
sherehe hizi zimefana kiasi hiki. Kwa niaba ya wageni wenzangu
nawashukuru, nasema hongereni sana.
Niruhusuni pia
niwapongezeni kwa dhati wafanyakazi wenzetu hodari waliotangazwa na
kuzawadiwa hapa leo.
Tuzo mlizopata leo
ni uthibitisho wa utendaji kazi wenu mzuri. Naomba hii iwe ni chachu na
motisha ya kuwafanya muongeze bidii zaidi kazini ili mwakani muendelee
kuwa wafanyakazi bora. Nchi yetu itajengwa na wafanyakazi kama ninyi
mnajituma na kufanya kazi kwa ufanisi na nidhamu kazini. Ni matumaini
yangu kuwa ushindi waliopata wenzetu hawa utakuwa kichocheo kwa
wafanyakazi wengine kuongeza bidii kazini ili mwakani na nao wawe
washindi na kupokea tuzo.
Maslahi ya
Wafanyakazi
Ndugu Wafanyakazi;
Baada
ya shukrani na pongezi hizo, sasa naomba mniruhusu niwaeleze hatua
tuliyofikia katika kutekeleza baadhi ya ahadi nilizozitoa kwenu mwaka wa
jana kwenye mkutano na viongozi wa Wafanyakazi na hotuba yangu kujibu
risala yenu. Nianze na uboreshaji wa mishahara na maslahi ya watumishi
wa umma.
Mtakumbuka
kuwa katika hotuba yangu ya Shinyanga nilisema kuwa serikali inatambua
kilio cha watumishi wa umma kuhusu mishahara na maslahi yao kwa ujumla.
Niliwaahidi mambo mawili katika kushughulikia tatizo hili. Kwanza ,
niliwaahidi kuwa licha ya nchi na uchumi wetu kukabiliwa na matatizo
kadhaa, bado watumishi wa umma watapata nyongeza ya mishahara katika
mwaka wa fedha 2006/2007. Pili kwamba, nitaunda Tume ya kutoa
mapendekezo kuhusu namna ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa umma
nchini.
Napenda
kuwaarifu kuwa tumetimiza ahadi yetu kwa mambo yote mawili. Katika mwaka
huu wa fedha yaani 2006/2007 tumeongeza mishahara ya watumishi wa umma
kwa asilimia 5 hadi 15. Tarehe 12 Mei, mwaka wa jana wiki mbili tu baada
ya kauli yangu pale Shinyanga, niliunda Tume ya Kuboresha Maslahi ya
Watumishi wa Umma.
Tume ya Kuboresha
Maslahi ya Watumishi wa Umma
Tume hiyo
iliyokuwa chini ya Ndugu yetu Deogratius Ntukamazina, ilikuwa na jukumu
la kupendekeza juu ya namna bora ya kuboresha maslahi ya watumishi
nchini. Ilitakiwa kupendekeza misingi, uwiano na taratibu katika
kufanya marekebisho ya mishahara ya watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na
mchakato mzima wa kuelekea kwenye kulipa mishahara inayotosheleza
mahitaji ya maisha (living wage). Kadhalika ilikuwa na jukumu la
kuangalia juu ya masuala mengine yahusuyo maslahi ya wafanyakazi kama
vile pensheni na mengineyo.
Tume ya
Ntukamazina ilianza kazi rasmi tarehe 01 Julai, 2006. Na kama ambavyo
wengi wenu mnafahamu Tume hiyo tayari imekamilisha kazi yake na
kunikabidhi rasmi taarifa yake tarehe 22 Januari mwaka huu.
Napenda
kuitumia nafasi hii kwa mara nyingine tena kutoa pongezi za dhati kwa
wajumbe wa Tume ya Ntukamazina kwa kazi nzuri waliyoifanya. Wamefanya
uchambuzi wa kina ulio yakinifu kuhusu hali ilivyo kwa upande wa maslahi
ya watumishi wa umma hapa nchini. Tume pia imetoa mapendekezo muafaka
ya namna ya kushughulikia suala zima la kuboresha maslahi ya wafanyakazi
wa umma nchini.
Serikali kwa
upande wake imekuwa inayachambua
na kuyafanyia kazi
mapendekezo mbali mbali ya Tume
// hiyo.
hiyo. Dhamira yetu ni
kutekeleza mapendekezo ya Tume hiyo, hatua kwa hatua, kadri uwezo
unavyoruhusu. Katika mwaka ujao wa fedha yaani 2007/2008 tutaanza
mchakato wa utekelezaji na kuendelea nao miaka ijayo.
Hivyo nawasihi
watumishi wa umma kuwa na subira na wazidi kufanya kazi kwa kujituma
zaidi ili kukuza uchumi na hivyo kuongeza mapato ya Serikali. Kukua kwa
uchumi na kuongezeka kwa mapato ya Serikali ndiko kutakakoongeza uwezo
wa Serikali kuboresha maslahi ya watumishi wa umma mapema zaidi.
Tukumbuke kuwa
nyama nyingi na maziwa mengi siku zote hupatikana kwa ng¨®mbe aliyenona
kwa kupata matunzo na malisho mazuri. Hivyo hivyo, ikiwa tutafanya
bidii katika kukuza uchumi, serikali itapata mapato zaidi kupitia kodi.
Serikali ikipata mapato zaidi ndipo itakapoweza kuboresha maslahi ya
wafanyakazi wake na kutimiza vizuri zaidi wajibu wake kwa taifa na
wananchi wake.
Kwa sababu hiyo,
naomba kukumbusha wajibu wetu sote, viongozi, wafanyakazi, wakulima,
wawekezaji na wananchi kwa ujumla wa kufanya kazi kwa bidii zaidi na
maarifa katika kukuza na kuendeleza uchumi wetu.
Maisha bora ya
Mtanzania yataletwa na kukua kwa uchumi. Na kukua kwa uchumi kutaletwa
na sisi wenyewe kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa; kila mmoja wetu
mahali pake pa shughuli aifanyayo.
Bodi za Mishahara
ya Kima cha Chini
NduguWafanyakazi;
Jambo la tatu
nililoahidi, linalohusiana na maslahi ya wafanyakazi katika sekta
binafsi. Nilizungumzia uharakishaji wa uundaji wa Bodi za Kisekta za
Kima cha Chini cha Mishahara. Nilielezea kutokuridhishwa kwangu na hali
ilivyokuwa mwaka wa jana na nikaiagiza Wizara ya Kazi, Ajira na
Maendeleo ya Vijana kuongeza kasi ya uundwaji wa Bodi hizo.
Nafurahi
kwamba tangu wakati huo kasi ya kuunda Bodi hizo imeongezeka na hali
inaleta matumaini. Tayari Bodi zimeundwa katika sekta nane yaani:-
¡ö Sekta ya Huduma
za Majumbani
¡ö Sekta ya Huduma
ya Biashara na Viwanda
¡ö Sekta ya Madini
¡ö Sekta ya Huduma
za Afya
¡ö Sekta ya Huduma
za Majini, Bahari na Maziwa
¡ö Sekta ya Huduma
ya Ulinzi Binafsi
¡ö Sekta ya Kilimo
¡ö Sekta ya
Usafiri na Huduma za Usafirishaji.
Nafurahi pia kuwa
kazi ya kutengeneza kanuni imekamilika na siku chache zijazo
zitazinduliwa.
Mchakato wa kuunda
Bodi kwenye sekta nyingine unaendelea kwa wadau, ambao ni pamoja na
waajiri na wafanyakazi, kutoa mapendekezo yao serikalini.Ni matumaini
yangu kuwa zoezi hilo litaharakishwa ili uundaji wa Bodi katika sekta
zilizobakia ufanyike mapema iwezekanavyo.
Ndugu Wafanyakazi;
Bodi hizi ni
muhimu sana katika mfumo wetu wa sasa wa kushughulikia maslahi ya
wafanyakazi nchini. Uamuzi wa mishahara na maslahi ya watumishi wa umma
hufanywa na Serikali. Zamani serikali ilikuwa inaamua hivyo kwa
wafanyakazi wote nchini hata wale wa sekta binafsi. Siku hizi,
utaratibu umebadilika. Maamuzi ya kima cha chini cha mishahara kwa
wafanyakazi wa sekta binafsi hufanywa na Bodi za Kisekta. Serikali
inalo jukumu la kuhakikisha kuwa bodi hizo zinaundwa na kuteua wajumbe
wake.
Nafurahi kusema
kuwa wajumbe wa zile Bodi nane zilizokwishaundwa wameshateuliwa na
kuanza kazi. Ombi langu kwa wajumbe wa Bodi hizo ni kwamba wajitahidi
kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu mapema iwezekanavyo. Kilio cha
maslahi duni kwa watumishi wa sekta binafsi ni cha kweli, tena ni cha
muda mrefu. Sasa fursa ya kuyashughulikia matatizo yao imepatikana,
naomba itumike vizuri mapema iwezekanavyo.
Ni ukweli ulio wazi
kuwa wafanyakazi katika sekta binafsi wanalipwa mishahara duni na
maslahi yasiyoridhisha hata kidogo. Kwa kawaida, kote duniani
wafanyakazi wa sekta binafsi wanalipwa vizuri zaidi kuliko wenzao wa
sekta ya umma. Mwelekeo siku zote huwa wafanyakazi wa umma kukimbilia
sekta binafsi. Hapa kwetu ni kinyume chake.
Ni jambo la
kusikitisha kuona kwamba baadhi ya waajiri kwenye sekta binafsi
wanawalipa wafanyakazi wao ujira mdogo sana ambao kwa kweli
unawadhalilisha. Mazingira ya kazi nayo si mazuri hata kidogo mambo
ambayo yanahitaji kurekebishwa.
Ni matumaini yangu
kuwa Bodi za Kima cha Chini za Kisekta zitasaidia katika kutafuta
ufumbuzi na matatizo hayo kutoka sekta binafsi. Aidha, ni matarajio
yangu kuwa Bodi hizo zitapata ushirikiano kutoka kwa waajiri na
wafanyakazi.
Waajiri wanao
wajibu wa kujali maslahi ya wafanyakazi wao pamoja na kujali lengo lao
la kupata
faida. Kupata faida kwa
kuwapunja mishahara wafanyakazi wao si sawa. Kwa kweli si jambo halali
hata kidogo. Nawaomba wajali maslahi ya wafanyakazi wao ili kuboresha
mahusiano baina yao . Naamini wakifanya hivyo mahusiano yao yatakuwa
mazuri.
Suala la Ajira
Ndugu Wafanyakazi;
Suala la
kukuza ajira tumelipa kipaumbele cha juu katika agenda ya Serikali
yetu. Ni moja ya ahadi kuu za CCM kwa Watanzania zilizotajwa katika
Ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu. Nilielezea mkakati wetu wa kukuza
ajira serikalini na katika sekta binafsi. Kadhalika nilielezea dhamira
yetu ya kuanzisha utaratibu wa kuwasaidia watu kujiajiri.
Katika hili,
kubwa tulilolifanya ni kuanzisha mpango wa mikopo ya wajasiriamali wa
shilingi bilioni 21 kwa Tanzania Bara yaani bilioni moja kwa kila mkoa.
Kiasi hicho kimeongezwa maradufu kutokana na maelewano yetu na
mabenki. Mpango huu
unawalenga hasa wanyonge kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu.
Kama tulivyokwishafafanua shabaha yetu ni kwamba watu waitumie mikopo
hiyo kuanzishia shughuli za uzalishaji mali na huduma zitakazowaongezea
kipato na hivyo kuinua hali zao za maisha na kupunguza umaskini.
Tulianza
kutekeleza mpango huu mwezi Januari 2007 na hadi sasa mwitikio wa
wananchi umekuwa wa kuridhisha sana . Watu wengi binafsi, vikundi vingi
na SACCOS nyingi zimejitokeza kuomba mikopo hiyo kiasi kwamba maombi
yamezidi fedha iliyotengwa kwa lengo hilo . Hii ni dalili nzuri
inayoonyesha dhahiri jinsi gani Watanzania tulivyo na kiu ya kujiletea
maendeleo na kuondokana na umaskini.
Serikali
itaendelea kuwasiliana na vyombo husika ikiwa ni pamoja na benki za NMB
na CRDB ili kuhakikisha kuwa mpango huu unafanikiwa na unawanufaisha
wananchi wanyonge walio wengi wakiwemo wafanyakazi wa hali ya chini.
Vile vile
tutaendelea kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuwavutia
wawekezaji wengi zaidi wa ndani na nje. Tutaendeleza zoezi tulilokwisha
lianza la kuondoa vikwazo vya kuanzisha na kufanya biashara nchini ili
wawekezaji wengi zaidi wa ndani na nje ya nchi yegtu wavutike na kuja
kuwekeza hapa nchini.
Kufanya hivyo
kutakuza ajira na kupunguza kilio cha watu wengi na hasa vijana.
Muelekeo ni mzuri tunachotakiwa kufanya ni kusimamia na kutekeleza kwa
ukamilifu na kwa dhati maamuzi yetu hayo. Sisi Serikalini tunafanya
hivyo, nawaomba wadau wengine nao watimize ipasavyo wajibu wao kwa
maslahi yetu sote.
Ajira ya Wageni
Kuhusu tatizo
la wageni kuajiriwa katika nafasi za kazi ambazo zingeweza kufanywa na
Watanzania, ninachoweza kuwaambia leo ni kuwa serikali imeendelea
kuchukua hatua za kuziba mianya iliyokuwa inasababisha ulegevu katika
kusimamia kanuni na taratibu zilizopo zinazohusu ajira ya wageni nchini.
Zoezi hilo ni endelevu.
Tutaendelea nalo hadi
mambo yatakapokuwa yametengemaa.
Aidha, tutaendelea
kuimairsha mafunzo ya kada ya kati hususani mafundi mchundo ambalo ndilo
eneo kulikoshamiri zaidi ajira za wageni hivi sasa. Nina hakika
tukiyafanya haya tutaweza kuondokana na tatizo hili ambalo limekuwa
likipigiwa kelele na watu wengi hapa nchini.
Napenda
kuwahakikishia wananchi kuwa serikali iko makini na itaendelea kuwa
mtetezi imara wa maslahi ya watu wake likiwemo hili la ajira. Tutazidi
kusimamia kwa ukamilifu sheria zinazowalinda Watanzania dhidi ya wajanja
wachache wanaotaka kutumia mwanya wa utandawazi kupindisha kanuni na
taratibu tulizojiwekea.
Ushirikishwaji wa
Wafanyakazi
Ndugu Wafanyakazi;
Serikali
inatambua umuhimu wa kuwapa wafanyakazi uhuru wa kutoa mawazo na
kushiriki katika maamuzi mbalimbali yanayohusu uendeshaji wa taasisi
wanazofanyia kazi.
Hii inatokana na ukweli
kwamba kuna kutegemeana kati ya waajiri na waajiriwa, na kati ya
Serikali, Waajiri na Vyama vya Wafanyakazi. Kwa kutambua umuhimu huu
serikali imeweka mazingira ya kisheria yanayowezesha utekelezaji wa
dhana hii.
Hivyo, napenda
kusisitiza rai yangu niliyoitoa mwaka wa jana kuwataka waajiri
kuwashirikisha ipasavyo viongozi wa vyama vya wafanyakazi katika vikao
mbalimbali vya utoaji maamuzi katika sehemu zao za kazi. Nafurahi
kwamba baadhi ya waajiri wametekeleza lakini wapo wengine bado. Narejea
tena kauli yangu ya kuwataka wale ambao bado hawajatekeleza wafanye
hivyo mapema iwezekanavyo. Nimemwagiza Waziri John Chiligati afuatilie
jambo hili kwa karibu zaidi.
Ndugu Wafanyakazi;
Mwaka wa jana
mlitoa kilio chenu kuhusu mapungufu ya Mfuko wa Akiba ya Uzeeni wa
Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa. Naliahidi kuchukua
hatua. Nafurahi
kuwaarifu kuwa tumetimiza ahadi yetu hiyo. Mfuko huo wa Akiba ya
Wafanyakazi sasa ni Mfuko wa Pensheni wa Wafanyakazi wa Serikali za
Mitaa kama ilivyo kwa mifuko mingine.
Hii sasa
inawahakikishia wafanyakazi wa Serikali za Mitaa mafao bora zaidi
wanapofika mwisho wa utumishi wao. Napenda kuwahakikishia kuwa, tuko
tayari kuchukua hatua zaidi na zipasazo kuboresha zaidi mfuko huo pale
panapostahili.
Malipo ya Mafao
ya Wafanyakazi wa iliyokuwa EAC
Ndugu wafanyakazi
na Watanzania Wenzangu;
Katika
kutambua na kuthamini haki za wafanyakazi na mchango wao mkubwa kwa nchi
yetu, Serikali tangu Julai 2005, imekuwa ikitekeleza ahadi yake ya
kuwalipa mafao wananchi waliokuwa wafanyakazi wa iliyokuwa Jumuia ya
Afrika Mashariki iliyovunjwa mwaka 1977. Zoezi la kuwalipa lilianzishwa
na Serikali ya Awamu ya Tatu na sisi tunaliendeleza.
Jumla ya fedha
zilizotengwa kwa ajili ya zoezi hili ni shilingi 117 bilioni. Kati ya
fedha hizo serikali imekwishatumia shilingi bilioni 115 kuwalipa
wastaafu 36,405 tokea zoezi lianze hadi kufikia tarehe 30 Machi, 2007.
Malipo ya
mirathi ya wastaafu waliokwishatangulia mbele ya haki yamekuwa
yakifanyika kwa kupitia mahakama mbalimbali nchini. Idadi ya mirathi
yote iliyokwishalipwa hadi sasa ni 7,666 yenye thamani ya shilingi 30.9
bilioni.
Aidha, kati ya
malipo yote yaliyokwishafanyika hadi sasa wastaafu 6,888 bado
hawajajitokeza na jumla ya shilingi 22.9 bilioni bado hazijalipwa kwa
sababu hiyo. Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wale wote wanaohusika
kujitokeza kuchukua malipo hayo ambayo ni haki yao .
Na kama katika
orodha tutagundua kuwa watu hawajalipwa, tutatafuta fedha tuwalipe.
Mikataba ya Madini
Ndugu Wananchi;
Jambo lingine
ambalo nililizungumzia mwaka jana lilihusu mikataba ya madini. Katika
hotuba yangu ya Shinyanga nilizungumzia haja ya nchi yetu kutazama
upya mikataba hiyo ili
tuweze kunufaika na rasilimali ya madini aliyotujaalia Mwenyezi Mungu.
Nilisema pamoja na kuthamini sana mchango wa Makampuni ya madini
yaliyowekeza hapa nchini, bado kuna haja ya kuweka utaratibu mzuri
utakaotuwezesha sisi wenye rasilimali nao tufaidike.
Aidha,
niliagiza Wizara ya Nishati na Madini ishirikiane na Wizara ya Sheria
na Katiba, Wizara ya Uchumi, Mipango na Uwezeshaji na Wizara ya Fedha na
makampuni husika kuangalia upya Sheria yetu ya Madini na mikataba
tuliyowekeana kwa lengo la kufanya marekebisho stahiki.
Katika
kutekeleza agizo hilo , Agosti 10, mwaka wa jana Kamati Maalum ya
majadiliano ya mikataba ya madini iliundwa. Kamati hiyo ilikuwa na
jukumu la kufanya mashauriano na Tanzania Chamber of Minerals and Energy
(TCME) kuhusu mfumo wa kodi katika sekta ya madini. Pia ilikuwa na
jukumu la kufanya majadiliano na makampuni ya madini yenye mikataba ya
madini na serikali kwa lengo la kurekebisha kasoro zilizopo.
Ndugu Wananchi;
Nafurahi
kuwafahamisha kuwa, majadiliano kati ya serikali na makampuni makubwa ya
madini hapa nchini yamekuwa na mafanikio. Tayari kampuni ya Barrick
Gold Tanzania Limited na Resolute Mines Tanzania Limited zimekubali
kuondoa kipengele cha kivutio cha asilimia 15 kwenye salio la gharama ya
uwekezaji katika migodi yao . Hatua hii itayafanya makampuni haya sasa
kulipa kodi ya mapato miaka michache ijayo tofauti na ilivyokuwa kabla
ya hapo ambapo yasingelipa kodi kwa uhai mzima wa migodi yao .
Mazungumzo
yanaendelea na makampuni mengine kufanya kama ilivyokuwa kwa makampuni
haya mawili. Muda si mrefu nchi yetu nayo itaanza kunufaika ipasavyo na
utajiri mkubwa wa dhahabu tuliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu.
Kampuni ya
Barrick Gold pia imekubali kuilipa serikali kiasi cha dola za Kimarekani
milioni 7.0 kwa mwaka kwa kila mgodi inaoumiliki kuanzia mwezi
Desemba, 2006 hadi mwaka
2010. Malipo hayo ni mbali na dola za Kimarekani 200,000 ambazo kampuni
hiyo na ile ya Resolute itazilipa kila mwaka Halmashauri za wilaya
ambako kuna migodi yake.
Hivi sasa
tunapitia Sera na Sheria yetu ya madini kwa lengo la kuzifanyia
marekebisho stahiki katika muda si mrefu ujao. Nia yetu ni kuwa na
sheria ya madini itayohakikisha kuwa pande zote mbili zinanufaika sawia
yaani sisi wenye rasilimali ya madini na makampuni ya uwekezaji yenye
fedha na teknolojia. Tunataka Sheria hiyo ituwezeshe kuwa na mazingira
ambayo Waingereza wanayaita ¡°win¨Cwin situation¡±, yaani wao
wanapata na sisi tunapata.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Nimeona leo
nisema hayo. Lakini, niwaahidi kuwa yale yote mliyoyasema kwenye risala
yenu tutayatafakari na kuyafanyia kazi kama tulivyofanyia kazi yale
mliyoyasema mwaka wa
jana. Napenda kuona kuaminiana na kushirikiana kunakuweko na kunazidi
kukua baina ya nguzo zetu za utatu yaani Serikali, Waajiri na
Wafanyakazi.
Naomba nimalize
kwa kuwashukuru tena kwa dhati wafanyakazi wote nchini kwa juhudi kubwa
mnazozifanya katika kuimarisha uchumi wa nchi yetu na kuhudumia watu
wake. Tunatambua, tunathamini na kuheshimu mchango wenu adhimu.
Ukiufananisha uchumi wetu na mwili wa mwanadamu, nyinyi ni uti wa
mgongo. Bila ya nguvu zenu uchumi wetu hauwezi kusimama wala kuimarika.
Hivyo, napenda
kumalizia kwa kuwahakikishia kuwa daima dumu serikali itawajali,
itaendelea kuwahudumia waajiri na wafanyakazi ili kwa pamoja waweze
kutoa mchango mkubwa zaidi katika kujenga uchumi ulio imara na taifa
imara lenye neema tele.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki
Tanzania !
Asanteni kwa
Kunisikiliza.