Lazima watu wafanyekazi hata ikibidi kutumia sheria ndogo
Maisha Bora kwa Kila Mtanzania ni pamoja na mkoa wa Pwani
WAZIRI Mkuu Edward Lowassa amesema kuwa haikubaliki mkoa wa Pwani uendelee
kubaki nyuma kiuchumi na kimaendeleo nchini na kwamba bidii ya kufanya kazi na
kilimo cha kisasa kitumike kubadili hali hiyo.
Alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara eneo la Kiparang’anda wilaya ya
Mkuranga katika siku yake ya pili leo (Jumapili Mei 6, 2007) ya ziara ya siku
sita ya mkoa wa Pwani.
Waziri Mkuu ambaye ofisi yake ndiyo inayosimamia Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa aliagiza kuwa ndani ya mwezi mmoja Halmashauri zote za Wilaya za mkoa wa
Pwani zikutane na kupanga mikakati ya kuondoa umasikini Pwani.
“Baadaye ya kupanga mikakati yenu wote viongozi wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya
na Mkuu wa Mkoa tutakutana kuona tunakwenda vipi…Lazima tuibadili hali hii,”
aliongeza.
Katika mkutano wake wa hadhara wa leo, Waziri Mkuu Lowassa alirudia alichokisema
jana (Jumamosi Mei 5, 2007) Kibaha alipoanza ziara hii kuhusu umasikini katika
mkoa wa Pwani.
Leo (Jumapili Mei 6) na jana (Jumamosi Mei 5) alitoa mfano wa pato la mwaka la
kila mtu ambalo kwa Pwani bado liko chini kwa kulinganisha na mikoa jirani yenye
mazingira yanayofanana na Pwani. Pato la mwaka la kila mtu Pwani ni Sh. 268,944;
Lindi Sh. 315,328; Morogoro Sh. 375,647 na Tanga Sh. 439,576.
“Pwani bado mko nyuma kiuchumi na kimaendeleo…Tumieni ardhi kubadili hali hii.
Ikiwezekana inabidi kutunga hata sheria ndogo ili kuwalazimisha watu wafanye
kazi” aliongeza katika mkutano wa Kiparanganda.
Waziri Mkuu Lowassa pia alikemea tabia ya kuwatia mamba wasichana wa shule na
kuwakatisha masomo yao. Alichukizwa alipoambiwa kuwa mwaka jana wasichana 42
waliokuwa shuleni walitiwa mimba na mwaka huu tayari 10.
Aliwataka viongozi wampe taarifa ni hatua gani za kisheria zimechukuliwa kwa
waliobainika kuwa wamewatia mimba wasichana wa shule pamoja na wazazi wa
wasichana hao walioficha kutoa habari hizo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka wananchi wa mkoa wa Pwani
watekeleze kuanzia Julai mwaka huu agizo la Rais Kikwete kuwa kila kijiji
kijenge zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya nchini kote.
Kabla ya mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu alipata taarifa ya Wilaya ya Mkuranga,
alifungua SACCOS ya walimu katika Chuo cha Ualimu Vikindu, alitembelea shule
mpya za sekondari za Vikindu na Kiparang’anda na kuona shamba la mfano la
mikorosho ya mbegu mpya la mstaafu wa jeshi, Yahya Athumani Kipira.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu pia alipokea hundi ya Sh. Milioni 64 kutoka
kampuni ya uchimbaji gesi ya Songas kwa ajili ya ujenzi wa sekondari Jambani (Sh.
Milioni 49.3) na nyumba ya walimu katika shule ya msingi ya Njopeka (Sh. Milioni
14.9). Pia alipokea mabati 500 kutoka kwa mfadhili Bw.Mutembei, ambaye ni
mmiliki wa shule ya Sekondari ya St. Mathey iliyopo Kongoe.
Waziri Mkuu ambaye alisema alivutiwa na ujenzi wa shule ya sekondari ya
Kiparang’anda alitoa Sh. Milioni 1 kwa ajili ya maendeleo ya shule na mipira
miwili, mmoja kwa wavulana na mwingine kwa wasichana, kwa ajili ya kucheza.
Jana (Jumamosi Mei 5, 2007) akiwa katika wilaya ya Kibaha, Waziri Mkuu alizindua
kiwanda cha kubangulia korosho cha Michael Lund Cashewnut Processing Centre
ambacho ni cha kikundi cha ushirika cha Uvuki katika eneo la Visiga.
Alisifu kikundi cha Uvuki kwa kubuni ushirika huo na kuongeza thamani ya korosho
kwa kuibangua kiwandani na kutaka maeneo mengine yanayolima korosho yaige
mafanikio ya kikundi hicho.
Mapema alitembelea kituo cha utafiti wa kilimo kilichopo Tumbi, Kibaha na kuweka
jiwe la msingi la sekondari ya Mwanalugali kabla ya kukagua shughuli za SACCOS
za kikundi cha Mlandizi.
Kesho (Jumatatu Mei 7, 2007) atatembelea wilaya ya Rufiji. Wilaya nyingine
atakazotembelea ni Mafia, Kisarawe na Bagamoyo kukamilisha ziara ya mkoa wa
Pwani.
(mwisho)