Katika gazeti lako la leo 4/8/2007, ukurasa wa mbele kuna habari yenye kichwa Kikwete amshambulia Banduka.
Ofisi ya Rais Ikulu, inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu habari hiyo, lakini pia Ofisi ya Rais inaamini kwamba mwandishi wa habari aliyekuwapo wakati Mkuu wa Mkoa akitoa taarifa ya mkoa kwa Rais ameiandika habari hiyo out of propotion.
Ni kweli kwamba mkuu huyo wa mkoa katika taarifa yake alimweleza Rais kuhusu matatizo ya uhaba wa ardhi unaowakabili wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro, na pia akaeleza pia juhudi mbalimbali zinazofanywa na uongozi wa mkoa kukabiliana na tatizo hilo.
Baada ya kuuliza maswali kadhaa ya kutaka kupata taarifa za kina juu ya tatizo hilo na juhudi hizo za mkoa, ndipo Rais alipoushauri na kuutaka uongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kufanya mazungumzo na viongozi wenzao wa mikoa mingine na kuangalia uwezekano wa kupata maeneo ya kuwapeleka wananchi hao.
Alisisitiza suala la maandalizi kwa maana ya kufanya mazungumzo na viongozi wa maeneo husika kabla ya kutoa matamshi ya kuwapa matumaini wananchi kwamba watapelekwa eneo fulani.
Ni katika msisitizo huo wa kuwataka viongozi kufanya maandalizi mazuri kwa kufanya majadiliano kati yao , viongozi wenzao na wananchi walengwa ndipo alipotoa mfano wa matamshi ambayo huko nyuma yaliwahi kutolewa Ndugu Banduka, wakati huo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani kwamba wananchi wapatao 46,000 wangehamia mkoani Pwani ili hali hakukuwa na maandalizi yoyote yaliyofanyika.
Rais aliutoa mfano huo wa Ndugu. Banduka kwa nia njema kabisa, na hata namna alivyoueleza mfano huo ulikuwa katika lugha nyepesi ambayo haikuonyesha kama kulikwa na dalili au hata chembe ya kumshambulia Ndugu. Banduka Kama Mwandishi alivyoeleza.
Ofisi ya Rais imesikitishwa sana na taarifa hiyo kwa namna ilivyoandikwa na hasa alivyoifanya kuwa habari kubwa na kichwa cha habari kinachoweza kusababisha chuki katika jamii bila sababu zozote na msingi.