Shein aagana na Balozi wa Misri
Guestbook
Tanzania, is a country on the east coast of east Africa.
 
JakayaKikwete.com
 »  Home  »  Habari Mpya  »  Shein aagana na Balozi wa Misri
Shein aagana na Balozi wa Misri
By Penzi Nyamungumi | Published  08/9/2007 | Habari Mpya | Unrated

Ushirikiano kwenye sekta ya kilimo na mifugo umeelezwa kuwa ni moja ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika kutekeleza dhamira ya kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Misri.

Akizungumza na Makamu wa Rais Ikulu leo balozi wa Misri anayemaliza muda wake nchini bwana Sabry Magd Sabry amesema ili kutimiza dhamira ya kuimarisha uhusiano Tanzania na Misri zinapaswa kuweka mkazo katika kupanua maeneo mapya ya ushirikiano.

Balozi Sabry aliitaja sekta ya kilimo na mifugo kuwa moja ya sekta inayoweza kuvutia uwekezaji kutoka nchini kwake na pia ushirikiano katika ngazi ya serikali.

Alifafanunua kuwa nchi yake imedhamiria kuongeza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na Tanzania kwa kushirikisha sekta binafsi na pia kuongeza ushirikiano katika nyanja ambazo nchi mbili hizo zimekuwa zikishirikiana ikiwemo ya elimu na mafunzo.

Kwa upande wake Makamu wa Rais Dk Ali Mohamed Shein alimueleza balozi Sabry kuwa uwekezaji katika sekta mbali mbali nchini ni jambo linalopewa kipaumbele na serikali kwani ni sehemu ya mkakati wa serikali kufanikisha mpango wa Taifa wa Kukuza na Kuimarisha Uchumi- MKUKUTA

“Kwa hiyo milango iko wazi kwa wawekezaji kutoka Misri na hatua hiyo inaweza kusaidia kuondoa uhusiano wa kibiashara usiowiana kati ya nchi mbili hizo”, alieleza.

Dk Shein alibainisha kuwa Tanzania na Misri zimekuwa na uhusiano mzuri tangu wakati wa viongozi wa kwanza wa nchi hizo hayati Gamal Abdel Nasser na Mwalimu Julius Nyerere.

Kwa hiyo alisisitiza haja ya kutekelezwa kwa ufanisi wa makubaliano mbali mbali yaliyoridhiwa kati ya nchi mbili hizo ili kudumisha uhusiano huo kwa manufaa ya serikali na wananchi kwa ujumla.

Makamu wa Rais aliishukuru serikali na wananchi wa Misri kwa misaada yake na kusisitiza kuwa misaada ya wakati wa shida imedhihirisha kuwa nchi hiyo ni rafiki wa kweli wa Tanzania.

Balozi Sabry ambaye amekuwepo nchini tangu mwaka 2003 alikwenda kumuaga Makamu wa Rais baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini na anatarajiwa kurejea nchini kwake hivi karibuni.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent

Verification:
Enter the security code shown below:
img


Add comment
Comments