Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Ali Mohammed Shein amesema mpango wa Taifa wa kuimarisha sekta ya kilimo nchini umelenga katika kuleta mapinduzi katika sekta hiyo.
Amesema mpango huo unatekelezwa hadi mwaka 2012 utalinufaisha pia zao la pamba ambalo ni moja ya mazao muhimu ya kilimo nchini
Dk Shein amesema hayo ofisini kwake Ikulu leo wakati wa mazungumzo yake na ujumbe wa shirika la Tanzania Gatsbuy Trust ulioongozwa na Mstahiki David Sainsbury. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mhe. Stephen Wassira
Mstahiki Sainsbury ni mwanzilishi wa shirika la Tanzania Gatsbuy Trust na mfadhili shughuli za shirika hilo kupitia mfuko unaojulikana kama Gatsbuy Charitable Foundation ulioko nchini Uingereza.
Dk. Shein alifafanua kuwa utekelezaji wa mpango huo unaojumuisha kuajiriwa kwa maafisa wengi wa ugani pamoja na kutoa mafunzo zaidi unatarajiwa kufikisha huduma za ugani katika ngazi za chini hivyo kuinua kilimo ikiwemo zao la pamba.
Kwa hiyo Makamu wa Rais amemshukuru mstahiki Sainsbury kwa msaada wake katika sekta ya pamba nchini pamoja na misaada yake katika maeneo mengine kama vile kupambana na umasikini,uhaulishaji wa tekinolojia pamoja na kusaidia makaazi ya bei nafuu kwa wasio na uwezo.
Dk Shein amemhakikishia Mstahiki Sainsbury kuwa serikali ya Tanzania itashirikiana na taasisi yake katika jitihada zake za kuinua sekta ya zao la pamba nchini ili sekta hiyo iweze kutoa mchango wake muhimu katika kuinua uchumi wa taifa.
Kwa upande wake Mstahiki Sainsbury alieleza kuwa ana matumaini makubwa kuwa sekta ya pamba inaweza kupiga hatua kubwa endapo itapatiwa watumishi zaidi wa huduma za ugani pamoja na uendelezaji utafiti katika sekta hiyo.
Alishauri mbinu shirikishi zitumiwe na watumishi wa ugani, wataalamu pamoja na watafiti katika kuwafikia walengwa wakubwa ambao ni wakulima.
Akiwa nchini Mstahiki Sainsbury alishiriki katika mkutano wa wadau wa sekta ya pamba uliofanyika katika hoteli ya Kilimanjaro Kempiski iliyopo jijini.