Serikali inakamilisha taratibu za kuandika mradi wa maji kwa ajili ya Maji
katika miji ya Masasi na Nachingwea na tayari mazungumzo ya kutafuta mfadhili
kwa ajili ya mradi huo wa maji kutoka katika chemchemi ya Ndanda yameshaanza.
‘Nimeshawasilisha maombi ya mradi huo wa maji na mazungumzo yanaendelea kati ya
Benki ya Maendeleo ya Uarabuni na Serikali, lakini pia Serikali inakamilisha
taratibu za kuandika mradi huu ili fedha za wafadhili zikichelewa tuanze wenyewe”
Rais Jakaya Kikwete amewaeleza wananchi wa Nachingwea katika mkutano wa hadhara
leo mchana akiwa katika ziara mkoani Lindi..
Tayari Serikali inagharamia mradi mwingine mkubwa kwa ajili ya huduma za maji
kwa wananchi wa Shinyanga na Rais Kikwete amesema amedhamiria kuleta huduma hii
kwa wananchi kama alivyowaahidi katika kampeni za kutafuta kura mwaka 2005.
“Napenda kuwahakikishia wananchi wote kwamba tumeomba kazi ya utumishi na
tumeianza, tunaendelea na tutaendelea nayo na kutimiza yale yote tuliyowaahidi
wakati wa kutafuta kura” amesema.
Rais Kikwete amesema Serikali imedhamiria kuboaresha huduma za jamii kama vile
elimu, afya, maji na miundo mbinu, pamoja na kuinua kipato cha wananchi ili
maisha yao yawe bora zaidi kuliko vile yalivyokuwa kabla ya Serikali yake
kushika uongozi wa Tanzania.
Akiwa mkoani Lindi kukagua shughuli za maendeleo na kuhakikisha kuwa ahadi
zinatekelezwa kama alivyoahidi, Rais Kikwete amewaagiza viongozi akiwemo Naibu
Waziri wa Miundo Mbinu Bw. Makongoro Mahanga, viongozi wa Wakala wa Barabara (TANROADS)
na uongozi mzima wa mkoa wa Lindi kuhakikisha kuwa barabara zote mkoani humo,
zinasimamiwa vilivyo ili zitengenezwe kufikia kiwango ambacho zitaweza kupitika
katika kipindi chote..
Rais ametoa maagizo hayo baada ya mkandarasi aliyepewa kazi ya kutengeneza
barabara mkoani humo kushindwa kuzikamilisha kwa muda na kiwango kinachotakiwa.
Rais amesema ni jambo la busara kama mkandarasi anashindwa kutimiza masharti
akanyimwa kazi nyingine badala ya kupewa kazi sehemu ingine, wakati
ameshadhihirisha kuharibu ile ya awali.
“Kama mkandarasi anashindwa kazi asipewe ingine ili wajifunze” Rais ameagiza.
Juhudi zingine za Serikali katika kutimiza ahadi kwa wananchi wa Nachingwea ni
pamoja na kuunganishwa na miji ya Lindi na Mtwara katika kupata umeme kutokana
na gesi ya Msimbati.
Serikali imeshatimiza baadhi ya ahadi katika wilaya za Mkoa wa Lindi ikiwa ni
pamoja na ujenzi wa shule ambapo wilaya ya Nachingwea sasa inaandikisha watoto
wenye umri wa kwenda shule kwa asilimia mia wilaya ina sekondari 14 na lengo la
mwaka huu ni kuwa na sekondari 26 ambapo inatarajiwa kuwa ifikapo mwishoni mwa
mwaka huu, shule zingine 12 zitafunguliwa.
Hata hivyo Mkoa wa Lindi pamoja na wilaya zake zinakabiliwa na tatizo kubwa la
watoto kupata mimba na kujiingiza kwenye mapenzi hivyo kufanya idadi kubwa ya
watoto kuacha shule kabla ya wakati.
Katika juhudi za Serikali kuinua maisha ya wananchi wake kwa ujumla, Serikali
imesema inaliwekea mkazo swala la ununuzi wa Korosho ili bei isiyumbe na
hatimaye kunufaisha wakulima.
Rais Kikwete amesema juhudi hizo ni pamoja na hatua ambayo Serikali imeshachukua
ya kurithi madeni ya vyama vya ushirika ili vyama hivyo viweze kukopesheka na
hatimaye bei ya korosho isiwe chini ya shilingi 610 kwa kilo ili mwaka huu
wakulima wafaidike na hatimaye kuinua hali ya maisha yao.
Mara tu baada ya kuwasili wilayani Nachingwea, Rais amepokea taarifa ya utendaji
ya wilaya ambapo pia amefungua nyumba za walimu wa shule ya msingi ya Mayaka,
amefungua ghala la mazao katika kijiji cha Litula kabla ya kuongea na wananchi
katika uwanja wa Sokoine.
Ghala la chakula la Litula ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa
Kilimo wa wilaya, shughuli ambayo inafanywa kupitia vikundi vidogo vidogo vya
uzalishaji ambavyo viliwezeshwa na Mradi shirikishi wa maendeleo ya kilimo na
uwezeshaji (PADEP).
Ghala hili litawanufaisha wakazi wapatao 1981 wa kijiji hicho ambao ni wakulima
kwa kiasi kikubwa.