Serikali imekikopesha Chama cha Ushirika cha Ilulu shilingi milioni 769 kwa
ajili ya ununuzi wa Korosho katika Mkoa wa Lindi.
Rais Jakaya Kikwete amewaambia wananchi wa Ruangwa leo asubuhi mara baada ya
kuwasili wilayani humo kuendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.
Mara baada ya kufika mkoani Lindi kuanza ziara Jumanne wiki hii na kuelezwa
matatizo ya ununuzi wa zao hilo kubwa la biashara mkoani Lindi, Rais aliwaahidi
wananchi kuwa atawatatulia tatizo la mikopo kabla hajamaliza ziara yake kwa
kuzungumza na Waziri wa Fedha ili pesa zaidi zitolewe kwa ajili ya ununuzi wa
Korosho.
“Nimeongea na Waziri wa Fedha kuhusu tatizo lenu hilo na ameniahidi kuanza kutoa
pesa hizo wiki hii ili muondokane na adha mnayoipata” Rais amesema.
Mapema Chama cha Ushirika kiliomba kukopeshwa shilingi bilioni 1.5 lakini
walipewa mil.731 ambazo mbali na kununua korosho pia zimetumika kununua vitabu,
magunia na usafiri hivyo hazikutosheleza mahitaji ya ununuzi na ndipo wananchi
wakatoa kilio chao kwa Rais na amewasaidia kutatua tatizo hilo.
Hata hivyo pesa hizi zinaonekana kuwa bado hazitatosheleza mahitaji yao hivyo
Serikali imeahidi kuwa kutoka sasa wataendelea kukopeshwa ili azma ya Serikali
ya kuwasaidia wakulima kujikwamua na kujiongezea kipato hatimaye itimie na
mkulima afaidike pia kwa kuuza kilo moja kwa shilingi 610 na hatimaye bei hiyo
iendelee kukua na kuimarika.
Rais Kikwete ambaye yuko mkoani Lindi na kufuatilia utekelezaji wa ahadi za CCM
kwa wananchi, Rais Kikwete pia amefungua rasmi daraja la Mbwemkuru juu,
linalounganisha wilaya za Ruangwa na Kilwa lililogharimu Halmashauri za Wilaya
hizo na Serikali Kuu milioni 166. Kabla ya kujengwa kwa daraja hilo, wananchi wa
wilaya hizo walikuwa wametengwa na mawasiliano kati yao yalikuwa magumu..
Daraja hili litawafaidisha wasafiri ambao hulazimika kupita Lindi wanaposafiri
kwenda Dar-es-salaam na pia wakulima ambapo sasa watasafirisha mazao yao kwa
wakati.
Rais amesema anafanya taratibu kuiingiza barabara inayopita katika daraja hilo
kwenye ngazi ya mkoa kutoka wilayani ili ifanyiwe mpango wa pesa na hatimaye
kufanyiwa marekebisho makubwa ipate kupitika wakati wote
Rais pia amezindua kituo cha afya Nanjilinji, nayo ni hatua kubwa za Serikali
katika kupunguzia wananchi adha ya kusafiri zaidi ya kilometa 5 kutafuta huduma
ya afya. Katika vituo hivyo vya afya vinavyotarajiwa kujengwa kote nchini,
huduma za ukunga pia zitatiliwa mkazo ili kuwaondolea adha wazazi na pia
kupunguza idadi ya vifo vya akina mama na watoto.
“Moja ya shabaha zetu kubwa ni kuendeleza huduma za afya nchini, tunataka kila
mwananchi apate huduma za afya zilizo bora, hivyo mwakani tunaanza mpango wa
kuwa na zahanati kila kijiji na kila makao makuu ya kata kuwe na kituo cha afya”
Rais amesema na kuwakumbusha wananchi kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Ukimwi
ambao hauna dawa.
Mara baada ya kuingia madarakani Serikali imeahidi kuleta maisha bora kwa
wananchi ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya, elimu, miundo mbinu na
kuinua hali ya kipato cha wananchi.
Tayari hatua kubwa imeshafikiwa katika ujenzi wa shule katika kila kata nchini
kote na tayari Serikali imeshaweka mipango ya kuanza ujenzi wa vituo vya afya na
zahanati karibu na wananchi wake.
Katika kuhimiza elimu bora na kwa kila mwananchi pale alipo, Rais Kikwete pia
amefungua majengo matatu ya maabara ya shule ya sekondari ya Mbekenyera wilayani
Kilwa na baadaye kuweka jiwe la msingi katika mradi wa nyumba za National
Housing Cooperation (NHC) huko Kilimahewa Ruangwa kabla ya kuzungumza na
wananchi katika mkutano wa hadhara.
Rais Kikwete amewahimiza wananchi kujenga shule za masomo ya Sayansi chini ya
Education II Project. Mradi huu umejumuisha ujenzi wa maabara 3, hosteli ya
kulala wasichana wapatao 20. Amewataka wananchi kujenga maabara kwenye shule
zote za sekondari ili wapatikane wataalamu wa kuleta maendeleo nchini.
Gharama ya ujenzi ni shilingi milioni 200 ambazo zimetolewa na African
Development Fund (ADF) ikiwa ni mkopo kwa Serikali ya Tanzania.
Rais ameahidi kuchangia shs. Mil. 10 kwa ajili ya kusaidia ukarabati wa mabweni
manne (4) ya wasichana na kuhimiza wazazi pia kujenga mabweni kwa ajili ya
wavulana ili watoto wengi waende shule.
Mkoa wa Lindi una matatizo makubwa ya watoto wa kike kupata mimba wangali
shuleni.
Rais Kikwete kesho ataendelea na ziara yake Lindi vijijini.