Hotuba ya Mama Kikwete kwenye maonyesho ya wasindikaji Mnazi mmoja
Guestbook
Tanzania, is a country on the east coast of east Africa.
 
JakayaKikwete.com
 »  Home  »  Habari Mpya  »  Hotuba ya Mama Kikwete kwenye maonyesho ya wasindikaji Mnazi mmoja
Hotuba ya Mama Kikwete kwenye maonyesho ya wasindikaji Mnazi mmoja
By Ikulu Press | Published  11/19/2007 | Habari Mpya | Unrated
 
HOTUBA YA MGENI RASMI / MHESHIMIWA MAMA SALMA KIKWETE, MWENYEKITI WA WAMA WAKATI WA KUFUNGUA MAONYESHO YA WASINDIKAJI YALIYOANDALIWA NA TAFOPA TAREHE 19 NOVEMBA 2007
 
 
Mlezi wa TAFOPA – Mama Regina Lowassa
 
Mwenyekiti wa TAFOPA – Bibi SUZY LAIZER
 
Wageni waalikwa
 
Mabibi na Mabwana
 
 

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru  kwa kunipa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika kufungua maonyesho haya ya usindikaji vyakula. Pili nawashukuru wanachama wa TAFOPA kwa kuandaa maonyesho haya muhimu.
 
Aidha naomba nitumie pia fursa hii kuwashukuru kwa dhati wafadhili waliowawezesha kufanikisha maonyesho haya. Msaada huu ni muhimu sana kwa wanachama wa TAFOPA kwa kuwa yanawapa fursa ya kujitangaza na sote tunafahamu kuwa kujitangaza ni moja ya mbinu muhimu sana za kuleta mafanikio katika Biashara.
 
 
 
 
 
Ndugu Mwenyekiti,
Uamuzi wa TAFOPA kuratibu na kufanya maonyesho haya ni jambo la kupongezwa sana. Ni dhahiri kuwa uzoefu katika kuandaa maonyesho haya utawezesha kuendelea kuandaliwa kwa maonyesho mengine ili kutoa fursa kwa wanachama na wajasiriamali wengine kutangaza bidhaa zao, kujitafutia masoko na pia kuwahamasisha watanzania kupenda bidhaa zinazozalishwa na watanzania ili kuinua uchumi wa Taifa letu.
 
Ndugu zangu wana TAFOPA
Binafsi nimefurahishwa sana na juhudi zenu za kuandaa kitu kizuri kama hiki. Hii ni changamoto kwa wajasiriamali wengine wadogo kujiunga na kutafuta nguvu ya pamoja katika kupata masoko. Hili linawezekana.
Ndugu zangu, kuna kitu kimoja ningependa kukisema bayana. Katika ulimwengu wa leo wa utandawazi kuna hatari ya wajasiriamali wadogo, kutupwa nje ya ulingo wa biashara kwa sababu ya ushindani mkubwa wa kibiashara unaowakabili.
 
Naamini wote mnatambua kuwa tunapozungumzia soko huria tunamaanisha haki na fursa sawa za masoko. Mlaji anayo hiari ya kununua bidhaa aipendayo bila ya kushurutishwa. Sasa ndugu zangu, nadhani kwa kuwa ninyi ni wafanayabiashara mnaelewa ugumu uliopo katika kushindana kibiashara baina ya ninyi wachuuzi wadogo na wazalishaji wakubwa wa viwandani.
 
Hii ni kwa sababu tofauti na wazalishaji wa viwandani, wajasiriamali wadogo wengi wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa mitaji na teknolojia ya chini wanayotumie hivyo kupunguza ubora wa bidhaa zao.
 
Hata hivyo ndugu zangu hilo lisiwakatishe tama. Kawa nilivyosema matatizo haya yanazo suluhu. Mbinu ya kwanza ni kujiunga pamoja kama hivi mlivyofanya ninyi, kwani sisi Waswahili tunasema “Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.”
 
Ndugu zangu wana TAFOPA,
Ni lazima mtafute ufumbuzi wa matatizo yenu kwa kuweka nguvu zenu pamoja. Muwekeze akiba zenu ndani ya SACCOS yenu ili muweze kukopeshana. Imarisheni umoja wenu mzidi kusonga mbele. Pia tengenezeni bidhaa bora zaidi ili muweze kumudu soko la ushindani.
 
Mwenyekiti TAFOPA,
Serikali inatambua umuhimu wa wasindikaji wadogo katika kukuza uchumi, wa Taifa, kutoa ajira na kuhifadhi mazao hasa wakati wa msimu wa mavuno. Kwa kutambua hii, serikali imeandaa sera na mikakati mbalimbali ili kuhakikisha kuwa inaweka mazingira mazuri, kuondoa leseni zisizokuwa za lazima ili kuwasaidia wajasiriamali wadogowadogo.
 
Lakini kama nilivyosema, pamoja na sera hizi nzuri za serikali, mwamuzi wa mwisho katika ununuzi wa bidhaa zako ni mlaji (mteja wako). Hivyo ni lazima muhakikishe bidhaa mnazozalisha ni za ubora wa kiwango cha juu kabisa ili kumvutia mlaji ili akila yeye asaidie kuwatangazia na wengine.
 
Ndugu zangu wana TAFOPA
TAASISI mbalimbali za fedha zimebuni mbinu za kuwasaidia wafanyabishara wadogo muweze kupata mikopo. Aidha kuna MKURABITA  na MKUKUTA ambazo zinajenga mazingira ya kisheria ya kuwawezesha kuanzisha biashara kirahisi. Na kama mlivyonieleza kwenye risala yenu wasindakaji wadogo mnaweza kupima bidhaa zenu na kupata nembo ya T.B.S. Bure.
 
Juhudi zote hizi ni kuhakikisha wazalishaji wadogo wanaimarika na kupiga hatua. Tanzania haina makampuni mengi makubwa ya usindikaji wa vyakula, hivyo mkombozi wa mazao ya shambani, hasa yale yanayoharibika kwa urahisi, kwa sasa ni huyu mjasiriamali mdogo. Na Serikali inatambua hilo.
 
Mwenyekiti,
Mimi ni mwenyekiti wa taaasisi isiyo ya kiserikali inayoitwa Wanawake na Maendeleo. Kazi yake kuu ni kuhamasisha na kusukuma mbele maendeleo ya wanawake. Nimejaribu kueleza juhudi za serikali kuendeleza wajasiriamali.
 
Lakini pia napenda niwakumbushe kuwa serikali yetu pia inatoa msukumo na uwezeshwaji wa makusudi kwa akina mama ili kuhakikisha hawaachwi nyuma kimaendeleo.
 
Nimalizie kwa kuwashukuru tena wafadhili wa maonyesho haya. Na sasa natamka rasmi kuwa maonyesho ya TANOFA ya usindikaji vyakula sasa yamezinduliwa rasmi.
 
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza
How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent

Verification:
Enter the security code shown below:
img


Add comment
Comments