|
Awahakikishia uwanja kukamilika mwezi wa nne
Rais Jakaya Kikwete amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Mafia kwamba, Serikali itamfuatilia na kumbana mkandarasi aliyepewa kazi ya kukarabati na kupanua njia ya kurukia na kutua ndege katika uwanja wa ndege wa Mafia.
Ametia uhakikisho huo jana (Jumatano) jioni wakati alipokuwa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara alioufanya wilayani huko katika siku yake ya nne ya ziara ya kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo mkoani Pwani.
“Kilio kikubwa cha wananchi wa wilaya hii, wabunge na wazee kiko katika mambo mawili- ghati na uwanja wa ndege. Na nilipofika hapa mara ya mwisho, wazee waliniambia bwana mdogo fanya yote lakini kwa hapa Mafia ni ghati na uwanja wa ndege ukiyafanya haya basi tutasema mmetimiza ahadi mliyoahidi, kweli kijana katimiza ahadi yake” akasema Rais na kushangiliwa na wananchi.
Akawaeleza wananchi waliokuwa wakimsikiliza kuwa nguvu za Serikali zimeelekezwa katika maeneo hayo mawili yaani uwanja wa ndege, na kwamba kazi ya ukarabati kama wanavyoona wananchi imeshaanza ingawa imechelewa kidogo.
“Nimekwenda kukagua ukarabati ule tukamuuliza mwenzetu vipi maana alishakuja mkandarasi mwingine hakufanya vizuri, sasa tukasema na huyu naye isije ikawa hadithi ile ile. Lakini huyu tutamsimamia, anasema tatizo lake saruji tumesema siye tutamsaidia labda asema lingine. Tena tutampatia Kasa ya Jeshi asafirishie na miye ndiye Mkuu wa Majeshi nitahakikisha inapatikana ili asiihamishe sementi kwenye miradi yake mingine”
Rais aliwafafanulia wananchi kuwa mkandarasi alipewa tenda hiyo B B Shaprya, ndiye pia amehusika katika ucheleweshaji wa mradi wa umeme wa gesi Somanga na ujenzi wa barabara ya Kipatimu.
Akabainisha kuwa awamu hiyo ya kwanza ya ukarabati na ujenzi wa njia ya kurukia na kutua ndege ambayo ujenzi wake unagharimu shilingi bilioni tatu, fedha ambazo zimetolewa na Serikali hadi sasa ukarabati wake umefikia asilimia 30 tu.
“Sisi tunataka awamu ya kwanza ya ukarabati huu ikamilike ifikapo mwakani mwezi wa nne. Kazi hii ikishakamilika tutaingia awamu ya pili ya kuuwekea lami uwanja huo, ili ndege kubwa zaidi zenye uwezo wa kubeba abiria 72 ziweze kuutumia uwanja huo bila matatizo” akaeleza.
Na kuongeza kuwa baada ya ukarabati wa awamu ya kwanza unaohusisha uondoaji wa tabaka la awali, kuweka tabaka la kwanza na la pili, kuimarisha msingi wa juu, kutengeneza mfumo wa maji ya mvua, ndege ndogo zisizozidi abiria 40 zitaweza kutua na kuruka bila matatizo.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete ambaye aliwafafanulia wananchi wa wilaya ya Mafia namna Serikali yao ilivyojipanga kuwaondolea kero na karaha wanazozipata kwamba, awamu ya pili ya ujenzi wa uwanja huo utagharimu shilingi bilioni 85, fedha hizo zitatoka Marekani kupitia mpango wa Millenia Challenge Account. (MCC)
Kazi zitakazofanyika katika awamu hiyo ni ujenzi wa jengo la abiria, jengo la kurushia ndege uwekaji wa lami, ukarabati wa maegesho, ununuzi wa gari za zimamoto, na kwamba tayari kazi ya usanifu ambayo imegharamiwa na Beki ya Dunia
Kuhusu ujenzi wa ghati, kero nyingine kwa wananchi wa Mafia, Rais amewahakikishia kwamba ghati hiyo itajengwa na kwamba shilingi bin. 2 zimeshatengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
“Kuhusu ghati taratibu zote zimekwisha kamilika, shilingi bn. 2 zimetengwa kwa ajili hiyo.Tunataka kuifungua Mafia iwe rahisi kuingia na kutoka lakini pia kuwawezesha wananchi wake kushirikiana na wenzao wa wilaya na mikoa mingine kwa urahisi, tunataka haya mawili (uwanja wa ndege na ghati) isiwe historia inayo jirudia rudia.
Alifafanua zaidi kuwa ghati za Kisiju na Nyamisati nazo zitajengwa ili kufanya mawasiliano kati ya maeneo hayo na Mafia kuwa mazuri zaidi. “Haya ninayoyasema si mambo ya kampeni, kampeni tulishamaliza, sasa tunatekeleza hadi zetu kwa vitendo tuwapendeje wana Mafia” akabainisha.
Kwa ujumla Rais alisema ameridhika na juhudi ambazo wananchi wa wilaya hiyo wanazifanya katika kuboresha maisha yao kuchangia sekta ya elimu, maji, afya na miradi ya ujasiriamali.
Akawashukuru wananchi kwa kumchagua yeye na Chama cha Mapinduzi ili kiweze kuwatumika na kuwaondolea kero zao, na kwamba Serikali imejipanga vizuri kwa kazi hiyo.
|