Raia Jakaya Kikwete amewasihi wanasiasa wenzake kuwahimizi wanachama wao kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa faida ya Watanzania wote.
Amesema katika jambo lolote linalohusu maendeleo, wananchi washirikiane pasipo kujali wapo katika Chama gani cha siasa, kwa sababu maendeleo hayana siasa.
“Ikijengwa zahanati haitamuhudumia mwana-CCM tu itamuhudumia kila mtu, vilevile kwa upande wa shule, barabara, miradi ya maji na mengine mengi. “Wanasiasa wenzangu tuendelee kusema na kwenye vijiwe vyetu, wewe hufai, mimi nafaa, wewe uko vile huyu yuko vile, lakini tutakapofika kwenye maendeleo yetu haya ni maendeleo kwa manufaa yetu sote” akasema.
Alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika wilaya ya Mafia akiwa katika ziara ya kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo mkoani Pwani.
“Tumeunda vyama vya siasa kwa sababu tunataka kuwaletea watu maendeleo, tunataka watu wapate barabara, wapate maji safi na salama, wapate huduma za afya kwa karibu na wapate elimu. Sasa pale tunapoendelea kushughulikia haya naomba sana sote tuungane kuyafanikisha” akasihi.
Ameeleza kuwa yule anayevutia upande mwingine huyo hana maslahi ya maendeleo ya watu, bali anatawaliwa na ubinafsi wake. “Tuondoe ubinafsi wetu ndugu zangu tujenge maendeleo yetu.”
Akasema tofauti za kisiasa miongoni mwa Watanzania kunawapa fursa ya kuchagua sera bora zaidi , akiona CCM inamfaa zaidi basi atakwenda huko na akiona CUF inamfaa zaidi atakwenda huko. “Lakini tusiichukulie fursa hiyo kuwa chanzo cha mifarakano katika jamii, ninachohimiza ni kujenga umoja na mshikamano wa kimataifa na kuwaletea wananchi maendeleo.
Akasisitiza kuwa chama chochote cha kiasa kinachopinga wanachama wao kushirikiana na wenzao kujiletea maendeleo yao , basi ni bora chama hicho kisiwepo kabisa
Katika mikutano yake mbalimbali aliyoifanya hapa Mafia, Rais Kikwete mara kwa mara alikuwa akiwasisitiza wananchi wa wilaya hiyo, kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kushirikiana katika kujiletea maendeleo.
Alitahadharisha kuwa kuendekeza malumbano ya kisiasa, na kukatazana kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo si tu kunawachelewesha wao wenyewe katika kujiletea maendeleo yao kwa kasi, lakini wataachwa nyuma na Watanzania wenzao katika maeneo mengine ya nchi.
Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Belen na kutoa shilingi Milioni moja kuchangia nguvu za wananchi katika ujenzi wa shule hiyo inayotarajiwa kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani. Hadi kukamilika kwake itagharimu shilingi million 200.
Rais pia aligawa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Tsh. Million 51 ambavyo vilitolewa na na Japani kupitia mfuko wake wa Maendeleo ya Jamii ( JSDF). Vikundi sita kati ya hivyo ni vya akina mama wanaojishughulisha na biashara ya kukaanga samaki na kazi za migahawa, na vilivyobaki ni vya uvuvi, kilimo cha miwa, na ukaushaji/uhifadhi wa samaki.
Vifaa vilivyotolewa kwa vikundi hiyvo ni injini 7 za kupachika, nyavu 14 za kuvulia, masanduku 102 ya kuhifadhia samaki, friji (deep freezer) kubwa 2, friji ndogo 1, vikaango vikubwa vitatu vya kukaangia samaki, meza 4 za kuchakatia samaki, viti 14, makasha 152, Oven moja ya mkaa.
Baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Rais Kikwete aliwataka wajasiriamali hao kuvitumia vizuri vifaa hivyo ili viweze kuwasaidia katika kuboresha maisha yao lakini pia utunzaji huu uwawezeshe kupata vifaa vingine kutoka kwa wahisani mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Kikwete amewataka Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri, kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo imelenga katika kuwainua wananchi kimaisha na kuwaongezea kipato.
Rais alisema haipendezi na wala haifurahishi pale Mkuu wa Mkoa au wa Wilaya na hata Mkurugenzi anaposhindwa kujua nini kinachofanyika katika eneo lake kuwasaidia wananchi wake ili wajipatie maisha bora.
“Hivi kwa nini mnababaika pale ninapowauliza niambieni ni miradi gani munayoitekeleza ya kuwaondolea umaskini wananchi iwe mmoja mmoja au katika vikundi mnababaika, yaani mnasoma tu kilichoandikwa kwenye taarifa zenu, lakini nikihoji tu basi mnachanganyikiwa tu, acheni kutoa taarifa za kwenye makaratasi, miradi inayohusu wananchi lazima muifahamu kwa kichwa” akasema Rais.
Na kusisitiza kuwa maisha bora kwa kila Mtanzania hayawezi kuja kwa kuwapatia fedha, bali ni kwa kuwaibulia miradi na kuwawezesha waiendeshe kwa ufanisi, wajipatie kipato chao, na hapo ndipo maisha bora yanapoanzia, sasa nyinyi kazi yenu nini” akahoji Rais.
Kauli hiyo ya Rais ilifuatia baada ya Mkuu wa Wilaya ya Mafia kushindwa kubainisha kwa uwazi ni miradi gani ambayo wameiandaa kwa ajili ya wananchi wake, hata alipoulizwa Mkurugenzi wa Halmashauri naye alibabaika, mpaka pale Mbunge wa Jimbo la Mafia Mhe. Abdulkarim Shahah alipojaribu kufafanua.