Mafuta Mbadala Kuipunguzia Gharama Serikali – Jk
Guestbook
Tanzania, is a country on the east coast of east Africa.
 
JakayaKikwete.com
 »  Home  »  Habari Mpya  »  Mafuta Mbadala Kuipunguzia Gharama Serikali – Jk
Mafuta Mbadala Kuipunguzia Gharama Serikali – Jk
By Maura Mwingira | Published  12/4/2007 | Habari Mpya | Rating:
* Awahakikishia Kivuko Cha Kisasa Wananchi Wa Utete
 Rais Jakaya Kikwete amesema uzalishaji wa mafuta mbadala (ethanol) utakapoanza, utaisaidia sana Serikali kupunguza gharama za kuagiza mafuta kutoka nje na hali kadhalika kupunguza gharama za bidhaa mbalimbali nchini.

Ili mradi huo uweze kutekelezeka  Rais amewaagiza viongozi wa mkoa wa Pwani kuipa ushirikiano wa kutosha kampuni ya SEKAB kutoka Sweden ambayo ndiyo inayotekeleza mradi huo ili iweze kufanikisha azma yake hiyo.

Alikuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara alioufanya leo asubuhi katika kijiji cha Mloka wilayani Rufiki muda mfupi kabla ya kuruka na kuendelea na ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo wilayani Mafia.

Amewaeleza viongozi hao wa Mkoa na wananchi hao kwamba mafuta hayo mbadala pia yatatumika katika mradi wa mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam.

“Ndugu wananchi, nimeona baadhi yenu mmevaa fulana zilizoandikwa SEKAB.  Hii ni kampuni kubwa ambayo imekuja kuwekeza katika wilaya yenu ya Rufiji na Bagamoyo ili kuendesha mradi mkubwa wa kilimo cha miwa kwa ajili ya kuzalisha mafuta mbadala.

Ninawaagiza uongozi wa mkoa na ninyi wananchi muipe ushirikano mkubwa kampuni hii” akasema.

 
Na kuongeza kuwa yeye binafsi anaiunga mkono kampuni hiyo kwani kufanikiwa kwake kutaisaidia sana Serikali katika uendeshaji wa shughuli zake.

Akafafanua kuwa tayari kampuni hiyo kutoka Sweden imeshakamilisha maandalizi ya ekari 20, 000 huko wilayani Bagamoyo na kwamba katika wilaya ya Rufiji imepewa ekari 100,000 kwa ajili ya uzalishaji wa nishati hiyo.

Ameeleza zaidi kuwa mradi huo wa mafuta mbadala ni muhimu sana kwa Watanzania katika kipindi hiki  wakati mchakato wa kutafuta mafuta katika maeneo mbalimbali ya nchi ukiwa unaendelea.

Akizungumza namna gani Serikali ilivyojipanga kuwaondolea kero mbalimbali wananchi wa Rufiki na kijiji cha Mloka, Rais akasema Serikali itanunua kivuko kipya kitakachotumika Utete na kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 100, magari 4 na tani 50 za mizigo.  

Zabuni ya ununuzi wa kivuko hicho itatangazwa mwezi huu na kwamba kivuko kinatarajiwa mapema mwakani kuwafikia wananchi wa eneo hilo.

Hivi sasa wananchi wa Utete ili waweze kuvuka kwenda ng’ambo ya pili ya mto wanatumia kivuko cha kamba.

Kuhusu ujenzi wa barabara, Rais ameeleza kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuzitengeneza barabara za wilaya ya Rufiji na vijiji kadhaa ili ziweze kupitika kipindi chote.

Kuhusu maji, Rais amewataka wananchi kijiji cha Mloka kubuni mradi mkubwa wa maji na Serikali itawasaidia na kwamba amefurahishwa kwa namna ambavyo kwa kutumia nguvu zao na mchango wa Serikali waliweza kukamilisha mradi wa maji uliogharimu shilingi milioni 28.0.

Akiwa katika kijiji hicho cha Mloka, Rais alifungua shule ya sekondari ya Mwaseni ambako aliahidi kutoa shilingi milioni moja ili kusaidia maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo na pia akatoa shs. Millioni 2 ili kusaidia ujenzi wa shule ya Dundumikazi inayoenndelea kujengwa katika kata ya Nangurungu.

Rais amewahakikishia wananchi kuwa Serikali imejipanga vizuri katika kuwatumikia, kuwaondolea kero zao zote na kuwapatia maisha bora.

Wakati huohuom Rais ametoa kadi 100 kwa wanachama wapya walijiunga na CCM, kati ya hao 63 wametoka Chama cha Wananchi (CUF).
How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent

Verification:
Enter the security code shown below:
img


Add comment
Comments