Msipokazania Elimu Mtabaki Kuwa Wavuvi Na Wakwezi-JK
Guestbook
Tanzania, is a country on the east coast of east Africa.
 
JakayaKikwete.com
 »  Home  »  Habari Mpya  »  Msipokazania Elimu Mtabaki Kuwa Wavuvi Na Wakwezi-JK
Msipokazania Elimu Mtabaki Kuwa Wavuvi Na Wakwezi-JK
By Maura Mwingira | Published  12/4/2007 | Habari Mpya | Rating:
 Rais Jakaya Kikwete amechangia  milioni mbili baada ya kufurahiswa na wananchi wa Kisiju Pwani  kwa uamuzi wao wa kuachana na siasa na kisha kwa pamoja wakakusanya nguvu zao na kujenga shule ya sekondari za kata.
 
Nimefurahisha sana na mafanikio ya elimu hapa kwenu, na hasa hili la kuachana na siasa na kuamua kujenga shule kwa ajili ya watoto wenu, mmenikuna kweli na mimi nawachangia shilingi milioni mbili, akasema Rais na kushangiliwa na wananchi”
 
Wananchi wa Kisiju Pwani  wamegawanyika katika vyama viwili ambavyo ni chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), kutokana na tofauti hizo za kisiasa ujenzi wa shule za sekondari za kata katika eneo hilo umekuwa ukisuasua baada ya viongozi wa CUF kuwakataza wanachama wao wasichangie.
 
Viongozi wa  vijiji katika eneo hilo wanatoka CUF lakini diwani, na mbunge wanatoka chama cha mapinduzi.
 
Akaihutubia mkutano wa hadhara Rais  akasema, “siasa zenu hapa zinafurahisha sana, uongozi wote wa vijiji uko mikononi mwa CUF, lakini ulipokuja Uchaguzi Mkuu mkaamua kufanya kweli, kura mkampa diwani wa CCM, na ubunge mkaipa CCM, na urais mkaipa CCM, sana uchaguzi ujao hata viongozi wa vijiji wapeni CCM, hii ndio siasa”
 
“Tupige siasa lakini watoto wetu waende shule huko nyuma  mlikuwa mkishindana sana kujenga shule kwa sababu ya siasa , CUF walikuwa wanahamasisha wanachama wao wasichangie ujenzi wa shule, sisi (CCM) tunazungumzia kasi ya kwenda mbele, wenzetu wanazungumzia kasi ya kurudi kinyumenyume. Maarifa gani haya, kwa sababu hata viongozi wenu wakuu Hamad na Lipumba wamesoma hadi chuo kikuu nyie mnataka kubaki nyuma mnasema siasa ya chama hamtaki kujenga shule” akasema.
 
Akasisitiza “ ndio maana katika ziara yangu ya mkoa wa pwani nilitaka kwa makusudi nifike hapa  Kisiju Pwani, ichukieni CCM lakini pelekeni watoto wenu shule, msipowapeleka hamuikomoi CCM mnawakomoa watoto wenu. Lakini sasa nimefurahi mmeamua na kuacha siasa zenu, vaeni mashati ya kijani, vaeni mashati ya blue, lakini inapokuja  katika ujenzi wa shule mashati yenu wekeni pembeni”
 
Akawataka wananchi wa eneo hilo  ambao sasa wanajenga sekondari yao ya pili na mkoa mzima wa Pwani, kuwakataa wanasiasa wanaowakataza wasichangie elimu kwa kuwa watu hao hawawatakii mema na wanataka kuwarudisha nyuma
 
Kikwete amewaeleza wananchi hao wa Kisiju Pwani kwamba  si jambo la siri kuwa wananchi wa mkoa wa Pwani wako nyuma kielimu kwa sababu ya kutothamini elimu.
 
“Sisi watu wa Pwani tunayo sifa  ya kutothamini elimu, lazima tuambizane ukweli, na nikiwaambia miye siwatukani, hili ni tatizo letu sote, hatuthamini elimu” akasisitiza.
 
Na kuwafafanulia kwamba mikoa ya Pwani hakuna wasomi wengi kama ilivyokatika mikoa mingine  hasa kule walikochangamkia elimu, na kuwaeleza kuwa kama hawatakazania elimu wataendelea kulalamika kwamba wanabaguliwa.
 
“Kama hamtakazania elimu, kama hamtapeleka watoto wenu, mtaendelea kulalamika kwamba mnaonewa, mnabaguliwa, na kikubwa zaidi mtaendelea kuwa wavuvi na wakwezi, hamuwezi kuendelea na sifa hii lazima sasa muamke “ akasisitiza.
 
Akabainisha kuwa wilaya ya Mkuranga itapata wawekezaji wengi wa kimataifa na hivyo kutoa fursa nyingi za ajira lakini wananchi wa wilaya hiyo wanaweza kuzikosa fursa hizo kama hawatakuwa na elimu ya kutosha na badala yake wataishia kufanya kazi za chini.
 
Ameeleza kuwa amepata matumaini mapya ya mwamko wa elimu kwa wananchi wa Mkuranga baada  ya kupata taarifa nzuri za uandikishaji watoto wenye umri wa kwenda shule ambao umefikia asilimia 96.
 
Hata hivyo alielezea masikitiko yake baada ya kupewa taarifa kuwa moja la tatizo linalowakabili wanafunzi wa kike wilayani humo ni lile la mimba, ambapo wanafunzi 81 waliacha msomo kwa ujauzito.
 Aliwataka wazazi na hasa wanaume kuwapa fursa watoto wa kike wasome hadi mwisho wa ukomo wao, badala ya kuwaoza mapema au kuwapa ujauzito.
 
How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent

Verification:
Enter the security code shown below:
img


Add comment
Comments