Rais Jakaya Kikwete amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dkt Christine Ishengoma na wakuu wake wa wilaya kusimamia kwa karibu zoezi la ununuzi mkoani humo badala ya kuviachia vyama vya ushirika peke yake.
Sambamba na kuwataka viongozi hao kusimiamia ununuzi wa zao hilo, Rais pia amevitaka vyama vya ushirika mkoani humo kutowakata wakulima fedha kwa ajili ya mfuko wa pembejeo, maadam hawawapati wakulima hao pembejeo hizo. Kwani kwa kufanya hivyo ni kudhulumu haki za wakulima hao.
Kikwete alitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tafauti (Jumatatu) jioni wakati akihutubia mkutano wa hadhara Kisiju Pwani na akizungumza na wakulima wa kijiji cha Kalole, wilayani Mkuranga .
“Tuachieni hili (la ununuzi wa korosho) tuwasaidie haitachukua siku nyingi fedha zitaongezwa nimeshazungumza na Mkuu wa Mkoa na wakuu wa wilaya kuwa kazi yao kubwa kwa sasa ni kusimamia ununuzi wa korosho kwa sababu wasiviachie vyama vya ushirika kwa sababu linagusa maslaji ya wananchi.
Akawahakikisha wananchi aliokuwa akizungumza nao kuwa kabla ya kumaliza ziara yake mkoani humo fedha za nyongeza zitakuwa zimewasili ili chama cha ushirika cha CORECU kiendeshe zoezi hilo kwa kasi zaidi.
Akasema kuwa tatizo la kusuasua kwa ununuzi wa korosho mkoani humo kunatokana na ukweli kuwa chama hicho kinakabiliwa na matatizo mengi yakiwamo ya upungufu wa fedha walizoomba benki ambazo haziwezi kununua tani 7000 za korosho zilipatikana katika msimu huu mkoani humo.
Akizungumza na wakulima wa kijiji cha Kilole aliposimama kuangalia ghala lililokuwa limehifadhi magunia ya korosho. Mkulima mmoja, Bw Twaha Islali Alimasi alimweleza Rais kuwa kwa misimu mitatu mfululizo wamekuwa akikatwa shilingi 20 kwa kila kilo wanayouza lakini hakuwahi hata msimu mmoja kupata pembejo hizo.
“Nimesikia tatizo la ununuzi wa korosho wilayani mkurunga ndio maana nikaamua kusimama hapa, kwa kweli hili la kuwakata fedha za pembejo halafu hamupewi pembejeo hizo hili si nzuri, hii ni dhuluma kwa wakulima lazima viongozi waache ” akasema Rais.
Akijibu hoja nyingine ambayo ilitolewa na mkulima huyo kwamba korosho zote zilizokuwa zikinunuliwa na vyama vya ushirika zilikuwa zikiuzwa katika daraja moja, kwa shilingi 488. badala ya utaratibu wa awali wa kutenganisha madaraja ambapo daraja la kwanza ni shilingi 610 na la pili 488. Rais aliikemea tabia hiyo na kuiita kuwa ni dhuluma kwa mkulima.
“Hili la kuchanganya madaraja sina maelezo nalo lakini nacho ni kitendo cha dhuluma, kila haki lazima iendane na wajibu, nitazungumza na Bodi ya korosho waje wakae na chama cha ushirika ili walithibitishe hili” akasema Rais.
Katika maelezo yake kwa Rais, Bw. Twaha Islali Alimasi huku akiwa ameshika risiti za makato ya michango mbalimbali, alimweleza Rais kuwa mapatano ya shilingi 20 kwa kila kilo kwa ajili ya pembejeo yanawaumiza sana wakulima na hasa ikizingatiwa kuwa pembejeo zenyewe hawazipati.
“Mhe Rais kwa mfano mimi nimekuwa nikikatwa shilingi 20 kwakila kilo ninazouza kwa ajili ya pembejeo, lakini pamoja na kukatwa huko pembejeo zenyewe hatupati, lakini mbaya zaidi katika hizo kilo ninazouzwa nakatwa pia shilingi 20 nyingine kwa ajili ya mfuko wa elimu, lakini pia mtendaji wa kijiji anataka nitoe shilingi 10,000, elfu tano za kwangu na elfu tano nyingine kwa ajili ya mke wangu kuchangia elimu, kwa kipato chetu hiki kidogo fedha kwa kweli ni nyingi mno na tunaumia tusaidie”.
Hata hivyo mkulima huyo alisema kuwa yeye binafsi hakatai kuchangia elimu na anakubali kuchangia elimu lakini michango yake ieleweke.
Hata hivyo Rais amewataka wakulima hao kutokataa kuchangia elimu kwa sababu ni kwa faida ya watoto wao. “Katika kuchangia elimu hili sina mzaha nalo, lazima mchangie elimu ili watoto wenu wasome, sisi huku Pwani tuko nyuma sana kwa elimu kwa sababu tuliisubiri serikali, wenzetu wa mikoa ya Kilimanjaro, Mbeya na Kagera wamesoma sana kwa sababu wakati huo nao walikuwa wakikatwa fedha za elimu kupitia kahawa zao” sasa na sisi lazima tukubali kukatwa ili watoto wetu wasome.