Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ameahidi kutoa vitanda kwa ajili ya wanafunzi wa kike wanaosoma katika shule ya sekondari ya magindu iliyoko wilayani kibaha mkoani pwani.
Mama Salma alitoa ahadi hiyo jana (Jumapili) mara baada ya Rais Jakaya Kikwete kuizindua rasmi shule hiyo yenye wanafunzi 120 kati yao wasichana wakiwa ni 61 na wavulana 59.
“Mimi ni mkereketwa na elimu na hasa elimu ya mtoto wa kike, na baada ya kutembelea mazingira ya shule hii, nitatoa vitanda kwa ajili ya wanafunzi wa kike” akasema mama Salma na kushangiliwa na wanafunzi hao na wakazi wa kijiji cha Magindu.
Mama Salma alikuwa amefuatana na Rais katika siku ya kwanza ya ziara ya mkoa wa Pwani kukagua na kuhimiza shughuli za maendele mkoani humo.
Akisalimia na wananchi wa Magindu, mama Salma aliwahimiza wanafunzi hao kuongeza juhudi katika masomo yao na kuepukana na vishawishi na kuupiga vita ukimwi.
Shule ya sekondari Magindu ambayo ni ya kata imejengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na mbunge wao Dkt Ibrahimu Msabaha na mfanyabiashara maarufu Bw. Bakhresa.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya shule hiyo, mwalimu mkuu Bi. E Shiloto alimweleza Rais Kikwete kuwa shule hiyo ina vyumba vinne vya madarasa vinavyotumika na, vyumba viwili vinaendelea kujengwa kupitia mpango wa MMES na viko katika hatua za mwisho.
Kwa upande wa nyumba za walimu, alisema iko nyumba moja na nyingine iko katika hatua za kuezekwa na nyumba nyingine itajengwa kupitia fedha zilizotolewa na MMES na hivyo kutakuwa na nyumba tatu. Na kwamba kuna hosteli tatu zenye uwezo wakuchukua wanafunzi 150, mbili zikiwa zimejengwa na mbunge wajimbo hilo , Dkt Msabaha.
Akielezea changamoto za shule hiyo alizieleza kuwa ni kutokamilika kwa jengo la utawala, shida ya maji ambapo wanafunzi wanalazimia kutembea kilomita nne kuyafuata, usafiri, umeme, upungufu wa walimu na vifaa vya kupikia chakula cha wanafunzi wa hosteli.
Pia alieleza kuwa shule haina maabara, maktaba, stoo, jiko na bwalo la kulia chakula na samani.
Akizungumza baada ya kuizundua shule hiyo, Rais aliwapongeza wananchi wa kujenga shule yao ya kata na hivyo kuwapa fursa watoto wao kupata elimu, aliwahimiza kuendelea na ujenzi ili kukamilisha majengo yaliyobakia.
Rais pia alimshukuru Bw. Bakhresa kwa mchango mkubwa alioutoa ambao umefanikisha ujenzi baadhi ya majengo ya shule hiyo.