JakayaKikwete.com - http://www.jakayakikwete.com/tanzania
Mama Lowassa ataka wahitimu kuacha uvivu
http://www.jakayakikwete.com/tanzania/articles/627/1/Mama-Lowassa-ataka-wahitimu-kuacha-uvivu/Page1.html
By Irene K. Bwire
Published on 12/8/2007
 
MKE wa Waziri Mkuu, Mama Regina Lowassa amewataka wahitimu nchini kuacha uvivu na kuwa wabunifu kama wanataka kuwa na maisha mazuri.

 MKE wa Waziri Mkuu, Mama Regina Lowassa amewataka wahitimu nchini kuacha uvivu na kuwa wabunifu kama wanataka kuwa na maisha mazuri.
 
“Kama mnataka kuwa na maisha mazuri ni lazima mchukie uvivu na mfanye kazi kwa bidii, muwe wabunifu kwani ubunifu husaidia kuongeza tija kazini na kupunguza gharama za uendeshaji.”
 
Ametoa wito huo leo mchana (Jumamosi, Desemba 08, 2007) wakati akizungumza na wahitimu 246 wa kituo cha Msimbazi VTC katika mahafali yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Msimbazi, jijini Dar es Salaam.
 
Mama Lowassa amesema ubunifu katika dunia ya leo ya utandawazi ni muhimu na bila kufanya hivyo nchi yetu itazidi kuachwa nyuma kimaendeleo. “ Muwe wabunifu katika kila kazi mnayokabiliana nayo iwe yako au ya kuajiriwa … mwajiriwa mbunifu ni dhahiri atamwezesha mwajiri wake kupunguza gharama na kuongeza mapato,” alisema.
 
Aliwahimiza kuwa na nidhamu katika kazi watakazokwenda kufanya kwani bila kuzingatia nidhamu watapoteza ajira na hata biashara zao. “Hata kama umejiajiri ni lazima unategemea wateja; bila nidhamu utapoteza wateja na ukikosa wateja maana yake hakuna biashara,” alisema.
 
Aliwataka pia wawe wavumilivu na waaminifu bila kujali cheo cha mtu, kabila wala umri. Alisema kukosa uaminifu ni tatizo kubwa katika jamii ya Kitanzania na hasa kwa wale wanaoajiriwa.
 
“Ukienda makazini, wale wanaotengeneza ‘line’ ndiyo wanasifiwa na kuonekana mahiri na wao wala hawaogopi kujitapa mbele za watu, lakini wale waadilifu na waaminifu huonekana wabaya.”
 
“Ninawaomba jengeni na dumisheni uaminifu katika kazi zenu ili muweze kuaminiwa kwa mambo makubwa zaidi na muhimu zaidi,” alisema.
 
Aliwataka vijana wanaohitimu wajihadhari na maambukizi ya virusi vya UKIMWi kwani ugonjwa huo hauna kinga wa la dawa na uwezo wa kujikinga uko mikononi mwao.
 
Mapema akitoa nasha kwa wahitimu, Mkuu wa kituo hicho. Padre Benedict Shayo aliwataka vijana hao wahimizane juu ya kujiepusha na maambukizi ya VVU na madawa ya kulevya kwani kundi kubwa linaloathirika ni la vijana kama wao.
 
Alisema kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 1962, chini ya Kanisa Katoliki, kimekuwa kinatoa mafunzo ya ushonaji, mapishi na uhazili kamili hatua ya kwanza, ya pili na ya tatu bila kubagua dini wala kabila bali lengo likiwa ni kumkomboa Mtanzania na hasa mwanamke.
 
Alitaja changamoto zinazokikabili kituo hicho kuwa ni ukosefu wa kompyuta, mashine za kupigia chapa (typewriters) na uwezo mdogo kwa baadhi ya wanafunzi ambao wanafanya vizuri kimasomo lakini wanashindwa ada na kununua vifaa vya masomo.