MAKAMU WA RAIS wa Cuba, Bw. Esteban Lazo Hernandez amesema jambo kubwa ambalo limemgusa na anaondoka nalo kutoka Tanzania ni jitihada ya Watanzania kupambana na maisha.
"Watanzania ni wepesi na wanajituma. Kila mahali nilipopita nimekuwa nikiona watu wakijishughulisha na kazi, iwe biashara, iwe viwanda (wakati niko njiani) au hata katika mapokezi kote nilikoenda... na hili limenigusa kwa namna ya pekee," alisema.
Ameyasema hayo jana jioni (Jumapili, 16 Desemba 2007) muda mfupi kabla ya kuondoka nchini wakati akifanya mazungumzo na Waziri Mkuu Edward Lowassa ambaye alikwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kumsindikiza.
Akielezea kuhusu ziara yake ya siku tano hapa nchini, Makamu huyo wa Rais alisema alifanya mazungumzo na viongozi mbalimbali na mambo ya msingi waliyojadili yalihusu sekta za afya, kilimo, utamaduni na michezo. Maeneo mengine maalum yalihusu vita dhidi ya UKIMWI na juhudi za kuhifadhi nishati (energy saving initiatives).
“Maeneo mengine tuliyojadili ni kuhusu ushirikiano baina ya Tanzania na Cuba ambao umedumu kwa miaka 45 na waasisi wake walikuwa Mwalimu Nyerere na Fidel Castro… na baadaye Che Guevara ambaye alikuja hapa wakati akienda Congo,” alisema.
Alisema wamejadili pia masuala ya umoja wakilenga mashirika ya kikanda (regional organizations), haki za binadamu katika bara la Afrika na Amerika ya Kusini, na matatizo yanayolikabili Bara la Afrika na hasa Umoja wa Afrika (AU).
Kuhusu mahusiano ya kichama, Bw. Hernandez alisema wamezungumzia namna ya kuboresha mahusiano ya kichama baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Kikomunisti cha Cuba (CPC).
Vilevile, Bw. Hernandez alisema alipata fursa na kuzuru kaburi la Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume na pia kuitembelea familia ya Mwalimu Nyerere ambako alifikisha salamu za kiongozi wa nchi yake, Bw. Fidel Castro. “Salamu hizi si kwa familia ya Mwalimu peke yake bali kwa Watanzania wote,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alimweleza Makamu huyo wa Rais kwamba Tanzania itaendeleza uhusiano wa miaka mingi ulioanzishwa na viongozi waasisi wa Tanzania na Cuba, Mwalimu Nyerere na Bw. Fidel Castro.
Alisema mambo yaliyojadiliwa wakati wa ziara yake yatazingatiwa ili kudumisha mahusiano ya nchi hizi mbili. “Ni muhimu kudumisha mahusiano baina ya nchi zetu… na hasa ushirikiano katika sekta ya afya, kilimo na michezo.
Makamu huyo wa Rais ambaye amemaliza ziara ya siku tano nchini, aliondoka jana jioni kuelekea Ethiopia ambako atafanya ziara ya kiserikali ya siku tatu.