Serikali Kumuenzi Losurutia - Lowassa
Guestbook
Tanzania, is a country on the east coast of east Africa.
 
JakayaKikwete.com
 »  Home  »  Habari Mpya  »  Serikali Kumuenzi Losurutia - Lowassa
Serikali Kumuenzi Losurutia - Lowassa
By Irene K. Bwire | Published  12/19/2007 | Habari Mpya | Rating:
 SERIKALI itayaendeleza mazuri yote yaliyonzishwa na aliyekuwa mbunge wa Kiteto, Benedict Losurutia ili kumuenzi mbunge huyo ambaye wakati wa uhai wake alipania kuwaendeleza wananchi wa  Kiteto.
 
Akitoa salamu za serikali katika mazishi ya marehemu Loosurutia yaliyofanyika nyumbani kwa marehemu, Kibaya wilayani Kiteto leo mchana, (Jumatano, 19 Desemba 2007) Waziri Mkuu, Edward Lowassa alisema  upatikanaji wa nafasi za elimu kwa watoto na vijana wa  Kiteto ilikuwa ni  ajenda  muhimu ya marehemu na aliisimamia kwa nguvu zake zote.
 
Mheshimiwa Lowassa alisema marehemu  Loosurutia alitilia mkazo zaidi elimu kwa watoto wa kike ili kuwasaidia wasichana wengi ambao walinyimwa haki yao hiyo ya msingi kutokana mtazamo  wa baadhi ya watu  katika jamii wa  kutoa kipaumbele  katika elimu kwa wavulana kuliko wasichana.
 
Alisema marehemu Loosurutia atakumbukwa na wananchi wa Kiteto kwa juhudi kubwa alizofanya za kuhakikisha kwamba umeme unapatika katika mji wa Kibaya ambao ni makao makuu ya wilaya hiyo.
 
Akisoma salamu za wabunge, Mwakilishi wa wabunge katika mazishi hayo, Mbunge wa Iramba, Mgana Msindai alisema  michango ya marehemu Loosurutia katika mijadala ya vikao vya bunge ilidhihirisha wazi kuwa  alikuwa na nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo  wananchi wa Kiteto na Taifa kwa ujumla.
 
Alisema haikuwa rahisi kwa mbunge kutoka nje ya ukumbi wakati Bw. Loosurutia alipokuwa akitoa mchango wake bungeni. Alisisitiza kuwa maneno yake bungeni yalionyesha wazi kuwa alikuwa amekomaa kisiasa  na hakuwa mnafiki kwani  hakuogopa kusema ukweli.
 
Akihubiri katika ibada ya kumwombea marehemu iliyofanyika kwenye kanisa katoliki, parokia ya Kibaya, Paroko wa Parokia hiyo, Padri Temu alisema wakati wa uhai wake, Bw. Loosurutia  alishiriki katika kazi nyingi za ujenzi wa  nyumba za ibada bila kubagua dini  au madhehebu.
 
Padri Temu alisisitiza kuwa marehemu Loosurutia hakusubiri kuitwa kushiriki katika shughuli mbalimbali  za maendeleo ya wananchi na zile za dini bali kila aliposikia alijitokeza na michango yake ya hali na mali na alilitaja kanisa katoliki  la Parokia  ya Kibaya kuwa ni ushahidi wa moyo aliokuwa nao marehemu wa kushiriki katika ujenzi wa nyumba za ibada.
 
Katika mazishi hayo yaliyoambatana na mvua, Waziri Mkuu Mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusufu Makamba na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Mary Nagu na Waziri wa Mipango, Uchumi an Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa walishiriki pamoja na mamia ya waombolezaji.
 
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Bw. Jeremiah Solomon Sumary, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bw. Henry Shekifu, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Bw. Vincent Parseko Kone, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bibi Amina Mrisho, Katibu wa Bunge, Bw. Damian Foka, wabunge, wakuu wa wilaya, wananchi na viongozi wa vyama vya siasa na Serikali.
How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent

Verification:
Enter the security code shown below:
img


Add comment
Comments